Michezo

Azam yapokea kichapo kibaya mbele ya KCCA nchini Uganda

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imekubali kipigo cha mabao 4-2 dhidi ya KCCA katika mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu ujao.

Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa KCCA, benchi la ufundi Azam FC la iliutumia kama sehemu ya kujiweka sawa baada ya mazoezi makali ya takribani siku 10 kambini nchini Uganda.

Azam FC ilianza vema mchezo huo kwa kujipatia mabao mawili ya haraka, ikianza kufunga la kwanza dakika ya tatu lililofungwa na nahodha Agrey Moris, kwa mkwaju wa penalti.

Penalti hiyo ilitokana na mshambuliaji wa Azam FC, Danny Lyanga, kuangushwa ndani ya eneo la 18 na nahodha wa KCCA, Timothy Awany.

Dakika ya sita, Lyanga alitupia bao la pili kwa shuti la chini akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na beki wa kushoto, Bruce Kangwa.

Kuelekea dakika 29 za mwisho za kipindi cha kwanza, KCCA ilifanikiwa kusawazisha mabao yote kupitia kwa Muzamiru Mutyaba dakika ya 16 na Awany dakika ya 45 na kufanya mchezo kwenda mapumziko kwa sare ya 2-2.

Azam FC ilirejea kipindi cha pili kwa kasi, dakika ya 48 Lyanga alikosa nafasi ya wazi baada ya kupiga shuti lililopaa juu ya lango akiwa ndani ya eneo la 18 kufuatia kupenyezewa pasi safi na Singano.

KCCA iliongeza mabao mengine mawili katika kipindi cha pili na kuhitimisha ushindi huo, yakifungwa na Allan Kyambadde na Patrick Kaddu.

Mara baada ya mchezo huo, Azam FC itashuka tena dimbani keshokutwa Jumapili kucheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa zamani wa Uganda, Express FC.

Kikosi cha Azam FC

Mwadini Ally, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Agrey Moris, Mudathir Yahya/Salmin Hoza dk 73, Joseph Mahundi/Yahya Zayd dk 86, Frank Domayo, Danny Lyanga/Ditram Nchimbi dk 85, Tafadzwa Kutinyu/Mbaraka Yusuph dk 71, Ramadhan Singano.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents