Michezo

Brazil kucheza na Taifa Stars

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amethibitisha ujio wa timu ya taifa ya Brazil nchini na kusema wako tayari kutimiza masharti yoyote watakayowawekea.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisi za Shirikisho hilo Karume, Ilala Dar es Salaam jana, Tenga alisema wamekuwa kwenye mazungumzo na Brazil kwa wiki moja sasa na taratibu zinaenda vizuri.

“Ni kweli Brazil watakuja lakini hatujamalizana nao bado, tumefikia hatua nzuri katika mazungumzo yetu hatujamalizana nao, kumalizana nao ni kuandikishiana mikataba, wanakuja lini, wangapi, tukimalizana nao ni jambo zuri hilo tutawaeleza,” alisema.

“Tunapenda waje na tumewaambia tuko tayari kama nchi kutimiza masharti yao, nasema hivyo kama nchi kwa sababu hili si la TFF peke yake kuna mkono pia wa serikali na tunashukuru kwamba inatusapoti sana…muwe watulivu tu kwa sasa tunda limeshaiva, lakini halijawa bivu kiasi cha kuchumwa, likiwa tayari basi tutalichuma,” alisema Tenga.

Tenga alisema wakishamaliza mazungumzo na Brazil watakuwa tayari kueleza watacheza mechi ngapi na timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Brazil itakuja nchini ikiwa safarini kwenda kwenye michuano ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kuanza Juni 11 Afrika Kusini.

Miamba hiyo ya soka duniani imepangwa Kundi G katika michuano hiyo mikubwa duniani, ikiwa pamoja na Jamhuri ya watu wa Korea, Ivory Coast na Ureno.

Itarusha kete yake ya kwanza Juni 15 dhidi ya Korea kwenye Uwanja wa Ellis, Park Johannesburg. Kwa muda mrefu kocha wa Stars, Marcio Maximo ambaye ni raia wa Brazil amekuwa akidai kuishawishi nchi yake kufanya ziara hapa nchini.

Mwanzoni mwa mwaka 2007 Stars ilifanya ziara ya mwezi mmoja Brazil. Endapo ziara hiyo ya Brazil itafanikiwa, Tanzania itakuwa imejitangaza kisoka zaidi, kwani wanamichezo wengi duniani watakuwa wakiifuatilia timu hiyo.

Katika viwango vya soka vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Brazil imeiacha mbali Tanzania, kwani kwa mujibu wa viwango vilivyotolewa Aprili 28, Brazil ipo namba moja, wakati Tanzania ni ya 108.

Viwango vipya vinatarajiwa kutoka leo. Katika hatua nyingine, Tenga ameisifu timu ya Taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ kwa ushindi wa mabao 8-1 dhidi ya Eritrea mwishoni mwa wiki.

Twiga Stars ilipata ushindi huo mnono katika mechi ya raundi ya pili kuwania kufuzu fainali za Mataifa Afrika kwa wanawake zitakazofanyika Afrika Kusini Oktoba.

“Tuwapongeze sana, sikumbuki kama timu ya taifa ‘Taifa Stars’, iliwahi kupata ushindi wa idadi ya mabao kama hayo huko nyuma, nasikia kuna kipindi tulishinda saba, lakini nilikuwa sijaanza kucheza bado, tuliwahi kuifunga Kenya mabao matano katika kufuzu fainali za Mataifa Afrika mwaka 1980 lakini baada ya hapo sikumbuki ushindi mnono kama huo.

“Kazi bado lakini kwa sababu hii ni mapumziko, kipindi cha pili ni kwenye mechi ya marudiano, nawaomba wadau wa soka wajitokeze kuifadhili timu hii,” alisema.

Wakati huo huo, tiketi 380 za kombe la dunia tayari zimeshafika na waliozinunua wanatakiwa kufika TFF kuchukua tiketi zao kuanzia leo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents