Habari

CHADEMA: Hatuna mgogoro

MBUNGE wa Tarime, Chacha Wangwe (CHADEMA) jana aliyameza maneno yake mbele ya waandishi wa habari na kukana taarifa zilizomhusisha yeye akikirushia tuhuma kadhaa chama chake.

na Tamali Vullu

 

MBUNGE wa Tarime, Chacha Wangwe (CHADEMA) jana aliyameza maneno yake mbele ya waandishi wa habari na kukana taarifa zilizomhusisha yeye akikirushia tuhuma kadhaa chama chake.

 

Katika siku za hivi karibuni, kuelekea uchaguzi wa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, mbunge huyo, ambaye alikuwa akiwania nafasi hiyo, alinukuliwa akikituhumu chama hicho kwa ukabila na matumizi mabaya ya ruzuku.

 

Chacha, ambaye alifanikiwa kuinyakua nafasi hiyo, jana alikana kuhusika na baadhi ya taarifa za vyombo vya habari na kueleza kuwa hakuna mgogoro katika chama hicho kama inavyodaiwa.

 

Wakati Wangwe akifanya hivyo, Baraza Kuu la chama hicho, nalo lilijibu tuhuma hizo na kueleza kuwa chama hicho hakina mgogoro na ruzuku ya sh milioni 60 inayopata kila mwezi haiwezi kukigawa, kwani chama kinaweza kuendeshwa bila ruzuku.

 

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu tuhuma mbalimbali dhidi ya chama hicho zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari.

 

“CHADEMA ni chama kimoja, hakijagawanyika na hatuna mgogoro wa aina yoyote. Kuna baadhi ya vyombo vya habari vilivyo karibu na CCM vinatumika kuandika mambo yasiyokuwepo.

 

“Kamwe chama hakiwezi kugombanishwa na ruzuku ya serikali, kwani kimefuzu bila ruzuku. Ruzuku inachangia asilimia ndogo sana katika chama… hata ruzuku ikifutwa, CHADEMA tutakwenda mbele,” alisema Mbowe.

 

Alisema sehemu kubwa ya fedha zinazotumika kukiendesha chama hicho zinatokana na michango ya baadhi ya viongozi na kwamba matumizi ya fedha ya chama yanawekwa wazi kwa kiongozi yeyote anayehitaji.

 

Akizungumzia tuhuma za kushamiri kwa ukabila ndani ya chama hicho, pamoja na kukanusha, Mbowe alisema kuwa chama chenye ukabila ni CCM, ambacho kina mawaziri wengi wanaotoka Mkoa wa Kilimanjaro, wakati Mkoa wa Kigoma hauna mwakilishi ambaye ni waziri.

 

“Mkoa wa Kilimanjaro una mawaziri wanane huku ukiwa na wakazi wapatao milioni 1.2, lakini Mkoa wa Kigoma ambao una wakazi karibu milioni 1.7 hauna waziri hata mmoja… mtu hupaswi kuzungumza kama huna takwimu,” alisema.

 

Hata hivyo, Daniel Nsanzugwanko, ambaye ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, ni Mbunge wa CCM kutoka Mkoa wa Kigoma. Pia, Christopher Chiza ambaye ni naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika naye anatokea Mkoa wa Kigoma.

 

Lakini, akitetea hoja yake, Mbowe alisema kuwa ingawa wabunge hao kutoka Mkoa wa Kigoma ni manaibu mawaziri, hawaingii katika vikao vya Baraza la Mawaziri, ambamo hujadiliwa masuala yenye kupanga mustakabali wa taifa na kuwa kazi yao kubwa ni kujibu maswali bungeni.

 

Wangwe alisema hoja nyingi zinazotolewa katika baadhi ya vyombo vya habari si sahihi na wakati mwinigine huwa hazijasemwa kama zinavyoripotiwa.

 

“Ndani ya chama lazima tuzungumze ili tulete changamoto kwa Watanzania kwa lengo la kujenga chama, lakini baadhi ya vyombo vya habari wanatoa hoja hizo ‘out of contents’ (nje ya mada) au wakati mwingine hazijazungumzwa kabisa,” alisema Wangwe ambaye amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Bara, kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Amani Walid Kabourou aliyehamia CCM.

 

Alisema kwamba dhana kwamba chama hicho kina mgogoro inapandikizwa na CCM kwa lengo la kutaka kuwasambaratisha.

 

“Ndani ya chama hatuna mgogoro, ila tuna mdahalo na tumejenga utamaduni wa kuzungumza, na mikakati yetu tunaiweka wazi, lakini baadhi ya vyombo vya habari wanaigeuza ili kuonekana kuna mgogoro,” alisema.

 

Alisema kama Makamu Mwenyekiti, atakuwa na ushirikiano na viongozi wengine kwa lengo la chama kushika madaraka, ili kutoa mfano kwa vyama vingine ambavyo vinafanya mambo yake kwa siri.

 

Akitoa taarifa ya Baraza Kuu la chama hicho lililokutana juzi, Mbowe alisema pamoja na mambo mengine, baraza limepokea, kujadili na kupitisha taarifa ya Katibu Mkuu.

 

Alisema Baraza Kuu limepokea na kutathmini ziara zilizowahi kufanywa kwa kutumia helikopta katika mikutano ya kuwashukuru wananchi, kuhamasisha uwajibikaji wa serikali na kujenga chama na kubaini manufaa yaliyopatikana kutokana na ziara hiyo kwa CHADEMA na kwa taifa.

 

“Baraza Kuu limetafakari gharama za ziara za helikopta na kuwianisha na ziara nyingine na kuazimia kwa kauli moja kuendelea na kutumia helikopta katika awamu nyingine ya ziara za CHADEMA kama ambavyo iliazimiwa pia na Mkutano Mkuu wa CHADEMA mwaka 2006,” alisema.

 

Alisema baraza hilo limeridhia matumizi ya helikopta, kwani si anasa na yana tija kwa Watanzania na ufanisi katika kuendeleza chama.

 

Mbowe alisema Baraza Kuu pia lilipokea, kujadili na kupitisha mpango kazi na bajeti kwa mwaka 2008 na kusema mpango kazi huo utahusisha shughuli ambazo zitafanywa pia na kurugenzi mbalimbali za chama katika masuala ya utawala, uenezi, habari, sheria, bunge, halmashauri, vijana, wanawake, wazee, rasilimali, oganizesheni, mafunzo na mahusiano ya kimataifa.

 

Aidha, baraza limeridhia umoja wa madiwani wa CHADEMA unaojumuisha madhumuni, uanachama, muundo na masuala mengine muhimu yanayohusu taratibu za umoja wa madiwani.

 

“Umoja huu ambao wanachama wake ni kila diwani wa CHADEMA, utawaunganisha madiwani wa CHADEMA vizuri zaidi katika kutekeleza wajibu wao katika maeneo wanayowakilisha na kwa chama kwa ujumla,” alisema.

 

Sambamba na hayo, pia baraza limeazimia chama kiendelee na ushirikiano wa vyama vya upinzani vya CUF, TLP na NCCR-Mageuzi kwa lengo la kudumisha demokrasia nchini, kuunganisha nguvu katika kutetea maendeleo na hatimaye upinzani kuweza kuchukua dola.

 

Pia baraza hilo limetoa ratiba ya uchaguzi mkuu wa CHADEMA utakaofanyika mwakani kuanzia ngazi ya vitongoji hadi taifa.

 

“Mwezi Januari mwakani utakuwa wa maandalizi. Februari na Machi kutafanyika uchaguzi wa vitongoji, Mei na Juni uchaguzi wa matawi na Oktoba mosi hadi 20 uchaguzi ngazi ya majimbo.

 

“Novemba 20 hadi 30 utakuwa uchaguzi ngazi ya wilaya na Desemba 5 hadi 10 uchaguzi ngazi ya mikoa,” alisema mwenyekiti huyo.

 

Alisema kuwa Kamati Kuu itakutana Desemba 12 mwakani, Baraza Kuu, siku inayofuata na Mkutano Mkuu utafanyika Desemba 14 mwakani.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents