Baada ya kukosa mikopo… Wanafunzi UDSM wafunga virago

BAADHI ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wameanza kufunga virago kurudi kwao, baada ya Bodi ya Mikopo kushindwa kuwakopesha.

Na Reuben Kagaruki


BAADHI ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wameanza kufunga virago kurudi kwao, baada ya Bodi ya Mikopo kushindwa kuwakopesha.


Mbali na wanafunzi hao kuondoka, imeelezwa kuwa wengine wanashinda njaa au kushindia maji na mkate, kutokana na hali ngumu inayowakabili kwa kukosa mikopo hiyo.


Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana, na Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), Bw. Julius Mtatiro, alipozungumza na waandishi wa habari.


Alisema wanafunzi 309 wenye sifa za kupewa mikopo na Bodi, wamenyimwa mikopo hali inayowalazimu baadhi yao kuanza kufunga virago na kuondoka chuoni hapo.


Alisema hadi sasa wanafunzi wawili mmoja kutoka mkoa wa Kagera na mwingine Kigoma, wameacha masomo na kurudi nyumbani kwa kukosa mkopo.


“Hii inasikitisha kuona mwanafunzi ananyimwa masomo kwa kigezo kuwa amejisajili kama mwanafunzi binafsi, wakati anakidhi vigezo vyote vya kupewa mkopo,” alisema Bw. Mtatiro.


Alitaja vigezo hivyo kuwa ni kuwa Watanzania, wana daraja la kwanza na la pili, walijaza fomu za kuomba mikopo, wote wamepimwa uwezo wao wa kiuchumi na kuonekana hawana uwezo wa kujilipia ada kwa kupata daraja A (yaani wasio na uwezo wa kujilipia) na wamesajiliwa kwa kufuata taratibu zote za usajili chuoni hapo.


Alisema kwa mara ya kwanza walikosa udahili kutokana na UDSM kupangiwa idadi ya wanafunzi watakaopata mikopo na nafasi hizo zilipokwisha chuo kilitangaza nafasi za usajili binafsi.


Bw. Mtatiro alisema nafasi hizo zilipotangazwa ndipo wanafunzi hao walipoomba na kulipa ada ya kuanzia wakiwa na matumaini ya kupewa mikopo baadaye na Bodi kwa sababu ya kuwa na sifa.


Alisema, pia hali hiyo ya kunyimwa mikopo imesababisha baadhi yao kuandika barua za kuahirisha masomo.


“Hata wanafunzi waliopo wanaishi maisha magumu…haya ninayoongea hayatokei mbali ni hapa hapa Mlimani, chuo kinachotegemewa na Taifa hili,” aliongeza Bw. Mtatiro.


Alisema inasikitisha kuona unyanyasaji mkubwa unaofanywa na mamlaka zilizopewa jukumu la kusimamia elimu ya nchi na haingii akilini, kuona kuna Watanzania wanaopewa mikopo na wasiopewa wakati wote wana vigezo sahihi.


Alifafanua, kwamba kigezo pekee kisheria cha kumnyima mwanafunzi mkopo ni pale anapopimwa uwezo wake wa kiuchumi na kupata daraja F linaloashiria kuwa na uwezo mkubwa kiuchumi.


Bw. Mtatiro aliuomba umma wa Watanzania kufahamu kuwa kuna Watanzania wanaoshindia mlo mmoja wa mkate UDSM kwa sababu ya kukosa fedha za kujikimu.


Alisema kibaya zaidi baadhi yao wametoka mikoani na hawana ndugu wa kuwasaidia Dar es Salaam.


Alisema DARUSO kama taasisi inayolinda na kutetea maslahi ya wanafunzi hao inaiomba Bodi ya Mikopo na Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, iharakishe kuwapa mikopo wanafunzi, ili waweze kuendelea na masomo yao, kwani ni Watanzania wenye haki zote kikatiba katika nchi yao.


Alisema DARUSO itahakikisha inawasimamia wanafunzi hao hadi mwisho, kwani ni haki yao kupata elimu bila kunyanyaswa, kwani inafahamika wazi kwamba Watanzania wenye uwezo kiuchumi wanasoma nje ya nchi na waliopo nchini ni maskini wanaohitaji kusaidiwa.


Gazeti ili lilipofika Ofisi za Bodi ya Mikopo kujua hatima ya wanafunzi hao lilielezwa kuwa msemaji wa suala hilo, Bw. Cosmas Mwasobwa, hakuwa ofisini.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents