Habari

Mabasi 200 ya kasi kuanza kutoa huduma Jijini

Serikali inatarajia kuingiza nchini mabasi 200 yaendayo kasi yatakayoanza safari zake kati ya vituo vya Kimara, Msimabzi hadi Kivukoni jijini Dar es Salaam.

Na Benny Mwaipaja, pst, Kyela



Serikali inatarajia kuingiza nchini mabasi 200 yaendayo kasi yatakayoanza safari zake kati ya vituo vya Kimara, Msimabzi hadi Kivukoni jijini Dar es Salaam.


Hatua hiyo imelenga kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.


Hayo yalisemwa juzi wilayani Kyela na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Bw. Israel Sekirasa wakati wa mkutano uliowahusisha wadau mbalimbali wakiwemo wabunge na viongozi waandamizi wa serikali kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa na Ruvuma.


Bw. Sekirasa alisema SUMATRA imekamilisha
mazungumzo ha Hazina Kuu ili wajumbe wa Bodi ya Benki Dunia wanaotarajia kukutana Aprili 25, mwakani, waweze kuidhinisha kiasi cha dola za Kimarekani milioni 86 zilizoombwa na serikali kwa ajili ya kuimarisha miundombinu.


Aliitaja miundombinu hiyo kuwa ni ujenzi wa barabara ya waenda kwa miguu pamoja na barabara ya mabasi yaendayo kasi itakayopita katika maeneo ya wilaya za Ilala na Kinondoni ambayo wamiliki wake wamekwishalipwa na serikali, fidia ya Sh. bilioni 10.


Alisema basi la kwanza litaanza kufanya safari zake Januari, mwaka 2010 hatua ambayo itayaondoa mabasi madogo madogo katikati ya Jiji.


Katika hatua nyingine, Bw. Sekirasa amesema anatarajia kupeleka mapendekezo kwa wadau ili huduma za kusafirisha abiria katika miji hapa nchini, yakabidhiwe makampuni badala ya kuendeshwa na mmiliki mmoja mmoja.


Alifafafanua kuwa, wamiliki wadogo wadogo wa vyombo vya usafiri watalazimika kujiunga katika makampuni hayo ambapo leseni zitatolewa kwa makampuni badala ya mmiliki mmoja mmoja.


“Wadau wakikubali, hatua hii itasaidia sana kudhibiti hali ya usalama barabarani kwa sababu mamlaka itakuwa na uwezo wa kuiwajibisha kampuni kuliko ilivyo sasa ambapo inakuwa kazi ngumu kumdhibiti msafirishaji mmoja mmoja,“ aliongeza Bw. Sekirasa.


Wakichangia katika mkutano huo, baadhi ya wadau waliishauri SUMATRA kuwashirikisha kikamilifu wadau wanaofanyakazi nao kwa karibu ili kukomesha ajali za barabarani na za majini pamoja na rushwa ndani ya Jeshi la Polisi kwa kuwa vinavyochangia ongezeko la ajali.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents