Habari

Nchi za Afrika zatakiwa kuwa na sauti moja kuhakikisha zinakuwa huru

MHADHIRI wa Masomo ya Kimkakati katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) Prof. Eginald Mihanjo amesema katika kuadhimisha miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU), kuna haja ya nchi za Afrika kuwa na sauti na nguvu moja ya kuhakikisha nchi hizo zinakuwa huru.

Akizungumza hayo juzi jijini Dar es Salaam katika Kongamao maalum lilioandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwaajili ya kujadili masuala ya ulinzi na Usalama kwa nchi za Afrika,Prof. Mihanjo alisema endapo nchi hizo zitahakikisha zinashikamana na kuwa huru zitasaidia kwa kiasi kikubwa hali ya utulivu na amani na kufanya milio ya risasi kutosikika mahali popote.

Alisema nchi za Afrika zimejikomboa kiuchumi licha ya changamoto za kiusalama zilizopo ambazo nchi hizo zikiungana na kuwa na sauti moja zitaweza kusaidiana kuwa huru.

”Tunapoongelea masuala ya mabadiliko yasiokuwa ya kikatiba katika nchi zetu,inapaswa tuyaondoe na kuweka nguvu za pamoja katika kuimarisha sekta za kijamii,”alisema na kuongeza

”Msingi wa uchumi ni wananchi hasa vijana baada ya kuhitimu elimu ya juu wawe na ajira n vigumu nchi kuwa na amani kama vijana wengi hawana ajira,”alisema.

Alisema zaidi ya asilimia 50 ya watu ifikapo mwaka 20250 watakuwa vijana hivyo ni muhimu kubeba kundi hili la vijana hususan walio chini ya miaka 25 kwa nchi za afrika kuhakikisha wanawekewa mazingira mazuri ya ajira.

Brigedia Jenerali Mstaafu, Paul Mella

Kwa upande wake Brigedia Jenerali Mstaafu, Paul Mella alisema jukumu la kulinda amani na kuhakikisha nchi za Afrika zinakuwa salama ni jukumu la kila mmoja na sio vya wanajeshi pekee.

”Nchi za Afrika zinahitaji kushirikiana katika ushirikiano wa nchi na nchi,kuhakikisha maeneo yote yenye changamoto za kiusalama zinatatuliwa kwa ushirikiano wa kikanda,”alisema na kuongeza

”Ushirikiano wa sisi kama Afrika ni njia mojawapo ya kupambana na matatizo mbalimbali ya kiusalama ,kwani dunia hii sio salama sana ni duniani ambayo ipo katika mpito ambapo inatoka katika dunia iliyotawaliwa na mfumo wa dola moja yenye nguvu na kwenda katika mfumo mwingine ambao ni pande mbili au tatu,”alisema.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye,alisema kongamano hilo limetoa nafasi kwa vijana wa chuo kikuu na watanzania kujifunza na kuuliza maswali yanayohusu ulinzi na usalama wa bara la afrika.

”Vijana kujifunza masuala ya ulinzi na usalama sio masuala mapya ni maendelezo ambayo yanafanyika katika bara la Afrika kutoka katika baraza na amani ambapo limeadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake,”alisema.

Alisema Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha ulinzi na usalama ni sehemu ya maisha ya watanzania,ndio maana kuna kipindi Serikali inatuma Jeshi katika nchi mbalimbali kuhakikisha ulinzi na usalama unapatikana.

”Hii ni fursa hata kwa vijana kutoka kwa vyuo vingine wanawajibu kama sehemu katika kuhakikisha ulinzi na usalama unapatikana,”alisisitiza.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents