Habari

Hizi ni kati ya sababu zinazochangia wasanii wapya wa bongo kuhit na wimbo mmoja na kupotea

Inawezekana huwa unajiuliza inakuwaje inatokea unamsikia msanii mpya anakuja na single ya kwanza ina hit sana kwa kipindi Fulani, anapata mashavu ya kutokea kwenye magazeti na TV kama amefanikiwa kutoa video halafu ghafla wimbo ukichuja humsikii tena.

mic2

Swali hili limepelekea mimi kutafakari kati ya sababu nyingi zinazopelekea hali hii, na baada ya kuzichambua hapa tutaziangalia chache kati ya hizo.

Nimeamua kuchagua kutotoa mifano na majina ya wasanii kwasababu ambazo ziko kwenye mabano ya makala hii so no names! ila mwisho tutakubaliana kwa kuwa utapata mifano yako binafsi kutokana na maelezo.

1.MAANDALIZI HAFIFU YA KUKAA KILELENI KWA MUDA ENDELEVU (SUSTAINABILITY)

Wasanii wengi wapya huwa na maandalizi makubwa ya kutoka, lakini yanakuwa hafifu kwa upande wa jinsi ya kudumisha ukubwa wa ‘brand’ hiyo katika game.

Nikisema maandalizi hafifu ya kushika nafasi na kuiendeleza namaanisha nguvu nyingi huwekwa katika wimbo ambao msanii anatarajia kuutoa, lakini nguvu ya kuendeleza ‘hits’ kama hiyo ya kwanza haitilii maanani sana mwanzoni.

Hii pia inachangiwa na utamaduni wa kawaida kuwa hata kama msanii amerekodi nyimbo tatu, huchagua wimbo mzuri zaidi utakaomtabulisha, na kuna imani potofu iliyokuwepo zamani kuwa ukishakuwa na jina tu (Ukishatoka) basi raia watakuelewa na ngoma itakayofuata kwa kuwa umeingia kwenye mfereji wa watu maarufu wenye mashabiki wengi.

Lakini ukweli ni kwamba mambo yamebadilika, sasa kiwanda cha muziki kimeongeza chujio la ziada, haliangaliwi jina siku hizi inaangaliwa kazi, na msanii aliyetoka anapata wakati mgumu wa kuendelea kujitetea kwa mashabiki wake kuwa anaweza kwa kuachia wimbo mwingine mkubwa kama ule ama hata zaidi ya ule, akiteleza tu anasahaulika linabaki jina tu na wimbo wake mmoja.

2.KUWA ‘SURPRISED’ NA MAFANIKIO YA MAPEMA/KUPANIC

Kuna tofauti kati ya kuridhika ama kubweteka na mafanikio na kushtushwa na mafanikio ya haraka uliyoyapata kwa wimbo mmoja. Kwa wasanii wapya kwa uchunguzi wangu kinachowaumiza kati ya hivi ni kuwa ‘surprised’ ama kushtushwa kiaina na mafanikio mapema ya wimbo mmoja tu.

Hii hasa inasababisha tatizo kubwa la kisaikolojia, ambapo msanii anakuwa kama ameshtushwa hivi na jinsi jina lake lilivyopanda ghafla bila kutegemea kufika hapo, sasa hapa kesi inayokuwa kwenye kizimba cha ubongo wake ni ‘inabidi kutoa ngoma kali zaidi ama kama hii, na vipi kama nikifeli kuifikia hii, itakuwa noma’.

Hali hii ni hatari kwa upande mmoja japo ni faida pia kwa upande mwingine kwa kuwa wanasema msanii atakaza zaidi. Sasa hapo katika kutafuta jinsi ya kukaza zaidi plus kushangazwa na mapokeo ya wimbo wake wa kwanza, anajikuta amepanic na anakuwa anahangaika kufanya ‘anadha’ hit bila kuwa na uhakika kama itakuwa hit ama vipi, au arudie style kama ile ama iweje (hasa kwa waimbaji),mwisho msanii anajikuta anafeli japokuwa ana uwezo.

Japo pia tumeshuhudia baadhi ya wasanii wanapopata mafanikio ya ghafla hugeuka kuwa gumzo kutokana na vitendo vya ajabu ajabu ambavyo huwa wanafanya baada ya kuukwaa ‘umaarufu’ na kuanza uhusiano wa karibu bila kuachana na ‘pesa’ na kuzaa mtoto wao ‘sifa’.

3.KUKOSA USHAURI SAHIHI NA KUPEWA MAONI CHANYA KINAFIKI

Wasanii wengi huwa na desturi za kuhusisha watu mbalimbali katika kuwashauri juu ya kazi zao jambo ambalo ni zuri kupata maoni ya watu tofauti kabla hujaamua kufanya jambo. Lakini matunda ya ushauri anaopata msanii yanategemea sana mti aliochuma matunda hayo.

Maoni hukusanywa kwa watangazaji, Djs, marafiki wa kawaida na watu wanaoaminika kuwa na ufahamu wa muziki. Mkusanyiko wa washauri hao unazaakitu ambacho hakina ‘TBS’ ya kuthibitisha ubora wa ushauri, hivyo kama msanii hatakuwa makini anaweza either kupuuzia ushauri wa maana au kuendelea na ushauri wa kupotosha ambao utachangia yeye kufanya maamuzi yasio sahihi, mfano juu ya wimbo anaotaka kutoa kama unasifa za kuhit au laa.

Kijiweni walipo watu wasio na uelewa mzuri kuhusu muziki zaidi ya kufurahia mdundo unavyoenda huwa wanapousikia wimbo utaskia ‘mwanangu hili ni boooonge la ngoma yaani lazima umkalishe hata mtoto Diamond kwa huu wimbo’.

Kibaya zaidi kuna baadhi ya washauri ambao hufahamu kabisa kuwa wanachokisema sio sahihi, lakini kwa kuwa ni watu wa karibu wa msanii huyo na wanajua anapenda kusifiwa na wao wanataka kuendeleza mahusiano mazuri na star huyo mpya, humpa maoni ya kinafiki ya kumsifia kwa ngoma ya pili anayotaka kuitoa na mwisho wa siku msanii na manager wake wanaweza kujikuta wamepigwa changa la macho na maoni hayo na kujikuta wanabumisha ngoma ya pili ya msanii husika.

Bahati mbaya asilimia kubwa ya wasanii wapya huchukia sana maoni hasi na wanaoyatoa hujikuta wakiitwa ‘ma-snitch’, wenye wivu n.k. hii hupelekea kupokea yale ya kinafiki ama yasiyo sahihi.

4.KUBADILI PRODUCER ALIYEKUTOA

Kuna wasanii wengi wachanga wanaohit na wimbo mmoja , wanakuwa wametengeneza hit kwa msaada mkubwa wa producer, kwa kuhangaishana kuwekana kwenye mstari wa uimbaji, na hata kujikuta wanarekodi kwa kuunga unga, kugombezana booth na usumbufu mwingine.

Hatua hii huwa inakuwa ni somo ambalo mwalimu na mwanafunzi wanakuwa wamezoeana na wanajua wanavyofanya kupata kitu kizuri na somo linakuwa linahamia hatua ya pili. Sasa msanii kama huyo akishatoka na huo wimbo wa kwanza kisha akahamia kwa producer mwingine atakaempokea kama star anayejua, matokeo yake wanafanya kitu tofauti kabisa kinachowaangusha mashabiki.

Na mara nyingi wasanii wanaofanya vizuri kwa hit mfululizo, kama walikuwa wapya kabisa kwenye mfereji wa muziki, namaanisha hawakuwa katika band wala kwaya fulani, ama kuimba kabla, huwa wanafanya kazi kadhaa na producers wao na kuiva kisha kuendeleza ukali wa kila kinachotoka.

Sijamaanisha ni lazima umng’ang’anie producer aliyekutoa, lakini kwa hali niliyoelezea hapo juu huwa inawagharimu wasanii wengi wapya kwenye game na kujikuta wanaohit na wimbo mmoja.

5.TIMING YA TUKIO HUTENGENEZA HIT YA MSIMU

Kuna kitu kinachoitwa ‘timing’ ambacho huwagharimu sana wasanii. Unaweza kutoa wimbo mkali lakini kwa kuwa hukuwa na timing na hukusoma alama za nyakati wimbo huo unapotea.

Lakini kwa upande mwingine baadhi ya wasanii hupata gap la kufanya hit ya kwanza kwa kutumia tukio, ama msimu fulani. Sasa wengi hujikuta baada ya tukio hilo kumpandisha anakosa ‘kick’ ya kumsogeza hatua ya pili.

Sitaki kutaja majina, lakini wapo wasanii wanaofahamika kwa kutoa wimbo wa kumdiss msanii fulani na ikahit kutokana na tukio lenyewe na ukali wa wimbo pia. Unaikumbuka ‘Usiulize’ ya Rado? Duh….Samahani ndugu msomaji nilisema sitaji majina hapa so fanya kama umeparuka hapo juu.

Kwa huu mfano sitakiwi kuendelea kuandika zaidi ya hapo, najua kama ni mfuatiliaji wa muziki basi kuna majina yanaingia kichwani. Si wapo wasanii wengi ambao walitumia tukio la Loliondo na kikombe cha babu kufanya ngoma?! Huwa inakuwa hivyo japo hizo hazikuhit sana.

6.KUSHINDWA KUTAMBUA UMUHIMU WA ‘BRAND’ YAKE MPYA NA KUJITANGAZA

Hapa kwenye ufahamu juu ya ‘brand’ ya msanii hasa mpya kuna udhaifu mkubwa sana kwa wasanii wa hapa kwetu. Msanii mpya ambaye amehit na ngoma ya kwanza huwa anasahau kuwa yeye ni bidhaa iliyoko sokoni na jina lake ndo linaiuza hiyo bidhaa, matokeo yake anajikuta akitaka publicity kama ya nanii na kwa kudanganyika anafanya utumbo ili aandikwe.

Hasara yake ni kwamba anaanza kutengenezewa chuki na washabiki wake taratibu na hata kuwapeperusha wawezeshaji ambao wangeweza kuwekeza kwenye jina lake hilo jipya, wengine huanza kuwapiga madongo mameneja wao wa kwanza na kuwatusi, sasa huyo anaefuata anaanza kuwa na mashaka kuwa huyu msanii ni ‘mwehu’ anaweza kunigeuka muda wowote na mimi. Ni bora kutunza ubovu wa huyo meneja/producer wa kwanza si lazima kumpaka kwenye media.

Kitu kingine ni hiki ambacho kilitajwa kwenye makala ya ‘Makosa 14 ya hatari yanayofanywa na wasanii wengi Tanzania’ iliyoandikwa na Skywalker wa Bongo5, kushindwa kujitangaza, msanii mpya anaweza kubweteka na kuichukulia poa mitandao ya kijamii, kutengeneza connection na wadau wa media kwa kuwapa maelezo pia ya moja kwa moja. Hii pia inapelekea kushindwa kutambua tofauti kati ya ‘bad publicity na good publicity’, sio ilimradi unatawala vichwa vya habari.

7.BAHATI

Bahati mi naweza kuichukulia kama ni imani tu kwa kuwa hakuna ushahidi ama kielelezo cha moja kwa moja kinachoweza kukuonesha kuwa hii ni bahati tu ndo imefanya huyu kahit, kwa kuwa kama ni kweli kuna bahati basi hata wasiojua kuimba ipo siku wangefanya hit kwa kuwa na bahati tu.! Lakini kuna wakati inabidi kukubali tu kuwa kuna wanaohit kwa bahati.

Unaweza kukuta wimbo fulani ambao siku ya kwanza kuusikiliza hata haukukuingia kichwani hata kidogo, lakini ulipata nafasi ya kuwa kwenye radio waves kwa kipindi kirefu na ukawa hit, na hata ukiusikiliza tena leo bado haukuingii kabisa kichwani.

Au hata kuna wakati mtu ambae ametoa hit fulani kali sana hadi leo akiimba humuweki kabisa kwenye list ya waimbaji,….eeh..kama fulani na fulani…yap…najua umepata jina hapo..ila mi sitaji ng’o (no names). Hiyo ndiyo naweza kuita bahati tu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents