Michezo

Kamati ya kusimamia ngumi za kulipwa yafafanua sakata la Hassan Mwakinyo kudai kusafiri bila kibali 

Kamati ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa nchini kupitia kwa katibu wake, Yahya Poli imekanusha kuwa bondia, Hassan Mwakinyo hakusafiri bila kibali huku ikisema kuwa  swala la viza ni jukumu la promota na wakala.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA WADAU WA NGUMI ZA KULIPWA TANZANIA

Ndugu waandishi wa habari,
Katika mkutano huu tutatoa ufafanuzi kuhusu suala la Hassan Mwakinyo.

1. UFAFANUZI KUHUSU SUALA LA HASSAN MWAKINYO
Kama mnavyokumbuka, majuma mawili yaliyopita nchi yetu ilipata sifa kubwa sana kwenye tasnia ya michezo hususan mchezo wa ngumi za kulipwa baada ya Hassan Mwakinyo kumpiga Sam Eggington kwa TKO raundi ya pili katika pambano la raundi 10 lisilo la mkanda lililofanyika tarehe 8 Septemba, 2018 huko Birmingham, Uingereza. Ushindi wa Mwakinyo, uliipeperusha vyema bendera ya nchi yetu.

Aliporejea kutoka Uingereza, Mwakinyo alipata mwaliko wa kufika katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku ya ijumaa tarehe 14 Septemba, 2018. Pamoja na kumpa pongezi, wabunge walimpatia zawadi kwa kulitangaza vyema taifa letu.

Mara baada ya kutoka bungeni, akiwa katika viwanja vya bunge, Mwakinyo alifanya mkutano na waandishi wa habari, pamoja na mambo mengine, alizungumzia safari yake ilivyokuwa mpaka amefanikiwa kupata ushindi. Mwakinyo aliueleza umma kwamba alipata changamoto nyingi kwenye safari hiyo kama vile kulazimika kukopa hela ya viza kutoka kwa mwanafunzi na kusafiri bila ya kibali na hivyo kulazimika kusafiri kama mkimbizi.

Kamati inapenda kutolea ufafanuzi suala la kibali na kwa uchache kuhusu suala la viza. Kwanza si kweli kwamba Mwakinyo amesafiri bila ya kupata kibali, wakala aliyekwenda na Mwakinyo aliwasilisha maombi yake ya safari hiyo ndani ya siku 7 kabla ya safari. Kamati iliyajadili na kupitia kumbukumbu mbalimbali za Mwakinyo pamoja na mpinzani wake na iliridhia kumwombea kibali ili aweze kusafiri kwa ajili ya pambano hilo. Maombi ya kibali toka katika Kamati kwenda katika Baraza la Michezo la Taifa (BMT) yaliwasilishwa tarehe 3 Septemba, 2018 kwa “maombi ya dharura” na tarehe 5 Septemba, 2018 Kibali kilitolewa na nakala yake kutumiwa wakala aliyewasilisha maombi hayo ndugu Rashid Nassor ambaye ndiye aliyesafiri naye siku hiyo hiyo.

Ndugu waandishi wa habari, naomba ikumbukwe kwamba, kwa mujibu wa Kanuni za BMT, maombi ya vibali vya kusafiri nje ya nchi kwa shughuli za kimichezo yanapaswa kuwasilishwa siku 14 kabla ya safari. Inapoonekana kwamba safari hiyo ina tija kwa mchezaji na taifa kwa ujumla, BMT hutumia busara na kutoa kibali nje ya muda kama ilivyofanya kwa Mwakinyo ambaye alipata kibali ndani ya siku 2 tu. Hivyo, napenda kusisitiza kwamba, Hassan Mwakinyo alipata kibali kama nilivyoeleza hapo juu na nichukue fursa hii kumwomba radhi Katibu wa BMT pamoja na watendaji wote kwa kadhia hii.

Vilevile, kwa kifupi, napenda ifahamike kwamba, suala la viza ni jukumu la promota na wakala/bondia mwenyewe na pesa hiyo huwa inarudishwa na promota wanapofika huko kwenye pambano. Hivyo, tunasikitika kwa changamoto hiyo aliyopitia kupata visa lakini tunaamini kuwa wamerudishiwa na labda wakala aliyekwenda naye ndugu Rashid Nassor anaweza kulitolea ufafanuzi zaidi.

Mwisho, Kamati inapenda kuchukua fursa hii kumpongeza tena Hassan Mwakinyo kwa ushindi wake na iko tayari kumshauri kuhusu mustakbali wake mara baada ya ushindi huo kama ataona inafaa.

Imetolewa na:

Yahya Poli
Katibu – Kamati ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa Tanzania.
17 Septemba, 2018

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents