Mitindo: Safari ya Mengi Miyanga, kutoka kuwa mpishi mpaka mwanamitindo (Picha)

Mengi Sylivester Miyanga ni Kijana anayefanya Kazi zake katika Tasnia ya Mitindo na kufanikiwa kushiriki katika Majukwaa kadhaa Makubwa ya Mitindo Nchini. Kabla ya kuwa Mwanamitindo, Mengi alikuwa akifanya shughuli zake kama Mpishi katika Mahoteli mbalimbali makubwa nchini.

Miyanga alizaliwa mwaka 1995 katika Hospitali ya Bombo mkoani Tanga akiwa ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watano, alipata Elimu yake ya msingi katika Shule ya Michungwani huku Sekondari akisoma katika shule ya Segera.

Alifika Dar es salaam kwa lengo la kuwa Mwana Mitindo mwaka 2014 akitokea Mkoani Tanga, alifikia kwa Mjomba wake eneo la Kawe, ingawaje baada ya kufika mjini hali haikuwa rahisi kama alivyotegemea, hivyo aliamua kujishughulisha na Kazi ya Upishi kabla ya Kujikita zaidi kwenye Mitindo.

“Nilianza kujishikiza na kujishughurisha kwa kufanya kazi hotelini kama Mpishi (Chef) kwa miaka mitatu mfululizo, sikutaka kukaa bila Kazi,Siku zote ukitaka kufanikiwa usikae tu nyumbani lazima ujishughulishe, nilifanya kazi hiyo wakati najipanga kutumia kipaji changu cha Mitindo” alisema Mengi.

Safari ya Miyanga katika Tasnia ya Mitindo ilianza rasmi mwanzoni mwa mwaka Jana na kufanikiwa kupata Kazi mbalimbali za Kimitindo zilizomuwezesha kumuweka katika ramani ya Mitindo Nchini.

“Nilipata shavu la kufanya tangazo na kampuni kubwa ya Simu Nchini, Naishukuru kampuni hiyo kwa kuniona mimi naweza kufanya Tangazo lao” Alisisitiza Mengi.

Mengi aliongeza kuwa alipata Taarifa kuhusu Tangazo hilo la Kampuni hiyo ya Simu kupitia Mtandao wa Whatsap, Taarifa hiyo ilikuwa inasema watu wenye Vigezo wanahitajika kufanya Tangazo katika Kampuni hiyo ya Simu ambapo Siku ya Usahili uliofanyika eneo la Victoria Makumbusho walijitokeza washiriki zaidi ya 200.

Anasema kuwa Baada ya Usahili siku moja alipigiwa simu na Kampuni hiyo na kuambiwa kuwa amechaguliwa kushiriki katika Tangazo hilo.

Akielezea namna alivyojiunga na Chuo cha Mitindo cha Yetu Afrika, Mengi anasema kuwa aliona tangazo kwenye Mtandao wa instagram lililokwenda kwa jina la ‘Ukivaa Unapendeza’ Katika Tangazo hilo walitafuta Mtu anayejua kuvaa na kupendeza ambapo vigezo vyao vilikuwa ni kuthibitisha ushiriki wako kwa kulipia gharama ya ushiriki na alifanya hivyo kuthibitisha ushiriki wake.

Shindano lilifanyika mwezi wa pili mwaka Jana maeneo ya Sinza na huko ndiko alipopata kufanikiwa kukutana na Mmshiriki mwenzie Mwanadada Rehema Marando ambae alimshauri aende shule ya mitindo ya Yetu Afrika kwa ajili ya kuongeza ujuzi wake zaidi.

Mwezi wa Saba mwaka Jana alifanikiwa kushiriki katika Jukwaa la Spring Summer lililofanyika katika ukumbi wa Black Point Kinondoni na kufanikiwa kumkutanisha na Mbunifu wa mavazi wa Lebo ya Fashion One, Aitwaye Nelson Thomas aliemtaka ajiunge nae.

Akizungumzia swala la Wanamitindo wa Kiume kufanya Tangazo la Bidhaa za Kike, Mengi anasema kuwa Swala hilo linategemeana na aina ya bidhaa ya Kike atakayotakiwa Mwanamitindo kuitangaza na Malipo ya Kazi yenyewe

“Swala hilo linawezekana lakini inategemeana na vitu viwili, Mkwanja unaolipwa na aina ya Bidhaa ya Kike unayotakiwa kuitangaza, kama ni bidhaa ya kawaida kama Begi naweza kufanya hivyo lakini kama ni Nguo za ndani siwezi kufanya hivyo” Alisema Mengi.

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW