Habari

Mkongo anaswa na bangi ya milioni 4/-

POLISI mkoani hapa inawashikilia watu wanne akiwamo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa tuhuma ya kupatikana na mapipa ya bangi

Gurian Adolf, Sumbawanga

 

 

 
POLISI mkoani hapa inawashikilia watu wanne akiwamo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa tuhuma ya kupatikana na mapipa ya bangi yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni nne.

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Isunto Mantage alisema kuwa tukio hilo lilitokea katika kitongoji cha Bangwe, Manispaa ya Sumbawanga ambako watuhumiwa hao wanadaiwa kuingiza bangi hiyo kutoka DRC.

 

Alisema kuwa mfanyabiashara huyo raia wa DRC, Kasongo Tchofa (30) amekuwa na kawaida ya kusafirisha mafuta ya dizeli kwenda Kongo na anapokuja nchini hupakia bangi katika mapipa hayo yenye ujazo wa gramu 200 kila moja.

 

Inaelezwa kuwa mfanyabiashara huyo husafirisha bidhaa hiyo kwa njia ya maji kwa kupakia kwenye boti na kushushia kwenye bandari ya Kirando ambako huyasafirisha kwa gari hadi mjini Sumbawanga anakouza kwa bei ya Sh 2,250,000 kwa wafanyabiashara ambao tayari anakuwa amewasiliana nao.

 

Alisema kuwa baada ya Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema waliandaa mtego uliomnasa Mkongo huyo akiwa na wenzake katika nyumba moja katika Kitongoji cha Bangwe.

 

Kamanda Mantega alisema baada ya kuhojiwa na polisi raia huyo wa Kongo alikiri kujihusisha na biashara hiyo haramu akidai kuwa bangi huipakia kwa kukata kitako cha pipa na kukiziba kwa kukichoma moto hali ambayo kwa haraka haraka ni vigumu kubaini kuwamo bangi.

 

Watuhumiwa wengine ni Elias Chaula (30), Hussein Mikidadi (18) na Rashidi Hamisi (22) ambao ni wakazi wa Manispaa ya Sumbawanga. Watuhumiwa hao wanahojiwa na polisi wakati uchunguzi ukiendelea kabla ya kufikishwa mahakamani.

 

 

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents