Habari

Shambulio la Marekani dhidi ya Jenerali wa Iran lilikiuka sheria za kimataifa – Wataalam wa UN

Shambulio la Marekani ambalo lilimuua Jenerali Qasem Soleimani lilikiuka sheria za kimataifa, wataalamu wa Umoja wa mataifa wamesema.

msafara uliokuwa umembeba Qasem Soleimani ulishambuliwa karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad

Soleimani alikufa pamoja na watu wengine tisa katika shambulio la anga karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq mwezi Januari.

Muwakilishi wa kitengo maalum cha Umoja wa mataifa kinachoangazia mauaji ya kiholela, Agnes Callamard, anasema Marekani haijatoa ushaidi wa kutosha kuhalalisha shambulizi hilo.

Marekani ilimshutumu kwa kuchochea ugaidi. Wiki iliyopita, Iran ilitoa waranti ya kukamatwa kwa rais wa Marekani Donald Trump na watu wengine 35 kwa shutuma za mauaji na ugaidi.

Qasem Soleimani alikuwa nani?

Tangu mwaka 1998, Meja Jenerali Qasem Soleimani ameongoza vikosi vya kikurdi nchini Iran- kitengo maalum cha jeshi la Iran (Revolutionary Guards) ambacho huendesha opareshani zake nje ya nchi.

Alikuwa kiungo muhimu katika mapambano ya kimkakati Mashariki ya kati kupitia vikosi vya Kikurdi, ambavyo vinaendesha oparesheni yake kwa ushirikiano na jeshi la ulinzi la Iran.

Jina lake lilianza kuwa maarufu alipopewa nafasi ya kuongoza kikosi cha Quds na kujenga ushirikiano wa karibu na kiongozi mkuu wa kidini Ayatollah Khamenei kiasi wakati mmoja ulamaa huyo alishiriki na kufungua dhifa ya harusi ya binti ya Jenerali Soleimani.

Meja jenerali Qasem Soleimani, na vikosi vyake vinafanya kazi chini ya kiongozi mkuu wa kidini, Ayatollah Ali Khamanei, badala ya kufuata muundo wa kawaida wa kijeshi wa Iran.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alitaja jeshi la ulinzi la Iran Revolutionary Guards na washirika wake vikosi vua Kikurdi kama shirika la kigeni la ugaidi mwezi April mwaka jana.

Jenerali Qasem Soleimani hakuwa anajulikana na wengi nchini Iran hadi mwaka 2003 wakati Marekani ilipoivamia kijeshi Iraq.Kamanda wanamgambo wa Iraq Abu Mahdi al-Muhandis (Kulia) aliuawa sambamba na Soleimani

Umashuhuri wake uliimarika hatua ambayo ilifanya maafisa kadhaa wa Marekani kutoa wito wa kuuliwa kwake.

Muongo mmoja na nusu baadae Soleimani alifikia kuwa kamanda maarufu wa vita nchini Iran kiasi akipuuza miito ya umma kumtaka aingie kwenye siasa.

Bwana Trump alimuelezea Soleimani kuwa gaidi namba moja duniani kote.

Alidai uongozi wa jenerali uliwalenga Wamarekani na kuwajeruhi pamoja na kuwaua mamia ya raia na watumishi wa Marekani miaka 20 iliyopita na jenerali huyo alifanya shambulio la roketi nchini Iraq mwezi Desemba na kumuua mkandarasi ambaye alikuwa raia wa Marekani.

Soleimani alikufaje?

Jenerali aliwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad akiwa katika ndege inayotokea Syria mapema Januari 3.

Alikuwa anaondoka uwanja wa ndege akiwa pamoja na maafisa wa juu pamoja na wanambo wa Shia ambao walikuwa wanaungwa mkono na Iran wakati kundi hilo liliposhambuliwa na ndege isiyo na rubani ya Marekani.

Miongoni mwa watu ambao waliuawa pamoja na Soleimani alikuwa Abu Mahdi al-Muhandis, naibu kamanda wa kundi la kijeshi lenye umaarufu mkubwa na mwamvuli wa jeshi la Shia.

Bwana Trump alisema, alitoa amri ya shambulio hilo la anga ili ‘kusitisha vita’ kati ya Marekani na Iran.

“Soleimani alikuwa amepanga mpango mbaya wa shambulio dhidi ya wanadiplomasia wa Marekani na wanajeshi wake, lakini aliuawa kabla ya kutimiza mipango” .

Siku tano baadae, Iran ilishambulia ngome mbili za jeshi la Iraqi zilizowahodhi wanajeshi wa Marekani. Na hakuna mwanajeshi wa Marekani aliyeuawa lakini zaidi ya watu 100 waliathirika na majeraha ya ubongo.

Ripoti ya wataalamu wa UN inasemaje?

Agnes Callamard amewasilisha ripoti yake siku ya Alhamisi katika baraza la Umoja wa mataifa kitengo cha haki za binadamu huko Geneva.

Ripoti yake inasema Marekani haijatoa ushahidi wa kutosha kuonesha kuwa Soleimani alikuwa amepanga shambulio la siri dhidi ya maslahi ya Marekani hasa nchini Iraq, kufanya hatua za haraka kuwa muhimu kuchukuliwa.

“Meja Jenerali Soleimani alikuwa kiongozi wa mikakati ya jeshi la Iran na matukio nchini Syria na Iraq. Lakini tishio la Marekani kuondoa maisha yake kabisa lilikuwa kinyume na sheria.”Bendera ya Marekani ikichomwa moto

Marekani imepokeaje ripoti hii?

“Ripoti hii inaminya haki za binadamu na kuwapa mwanya magaidi kufanya wanachotaka na kwa mara nyingine hatua hii inathibitisha tena kwa nini Marekani ilikuwa sahihi kuondoka katika baraza la umoja wa mataifa linaloangazia haki za binadamu mwaka 2018,alisema msemaji wa mambo ya nje wa Marekani Morgan Ortagus.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents