Michezo

Stars yabanwa Taifa

Timu ya Soka ya Taifa, Taifa Stars jana ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Timu ya Taifa ya Malawi katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja mpya Dar es Salaam

Kiungo mshambuliaji wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Mrisho Ngassa (kushoto) akiangalia namna ya kumtoka mlinzi wa timu ya Taifa ya Mawali, Wisdom Ndhlovu wakati timu hizo zilipochuana katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki uliochezwa katika uwanja mpya wa taifa jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Henry Joseph wa Taifa Stars. (Picha na Mroki Mroki).
Kiungo mshambuliaji wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Mrisho Ngassa (kushoto) akiangalia namna ya kumtoka mlinzi wa timu ya Taifa ya Mawali, Wisdom Ndhlovu wakati timu hizo zilipochuana katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki uliochezwa katika uwanja mpya wa taifa jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Henry Joseph wa Taifa Stars. (Picha na Mroki Mroki).

 

 

 

Betram Lengama

 

TIMU ya Soka ya Taifa, Taifa Stars jana ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Timu ya Taifa ya Malawi katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja mpya Dar es Salaam.

Mechi hiyo ilikuwa ya kimataifa ya kirafiki, ambapo timu zote ziliitumia kujiweka sawa kwenye mechi za awali kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia na zile za Mataifa Afrika zitakazofanyika Afrika Kusini na Angola mwaka 2010.

Mechi hizo za awali zinatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii na Stars itaanza kete yake nyumbani dhidi ya Mauritius katika mechi itakayochezwa kwenye uwanja mpya.

Mechi hiyo ilikuwa ya vuta nikuvute na hasa kipindi cha kwanza ambapo Stars ilionekana kutawala na kulishambulia lango la wapinzani wao kabla Malawi haijachachamaa katika kipindi cha pili.

Katika kipindi hicho, Malawi ilishambulia lango la Stars kwa muda mrefu na kufanya mechi ichezwe nusu uwanja na hapo ndipo ilipopata bao la kuongoza.

Bao hilo lilifungwa katika dakika ya 54 na mchezaji anayecheza soka ya kulipwa Urusi Essau Kanyenda baada ya kuunganisha pasi kutoka kwa Moses Chavula kabla ya kuachia shuti lililojaa wavuni.

Kuingia kwa bao hilo kuliifanya Stars kubadilika kidogo na katika dakika ya 79 ikapata bao la kusawazisha kupitia kwa Salum Sued.

Mfungaji alifunga bao hilo baada ya kuwazidi akili mabeki wa Malawi waliokuwa wakielekea kuokoa mpira kabla ya kuingia katika himaya ya mfungaji na bila ajizi akafunga bao la kusawazisha.

Stars ingeweza kupata bao la pili katika dakika ya 86 pale beki Nadir Haroub ‘Canavaro’ alipokuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga lakini akapiga shuti lililogonga mwamba kabla ya kuokolewa na beki wa Malawi.

Akizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Stars Marcio Maximo alisema mechi hiyo ni majaribio tosha na timu yake imepata mazoezi ya kutosha tofauti na mashabiki wa soka walivyokuwa wakidhani.

Hata hivyo, pamoja na matokeo hayo, mashabiki waliojitokeza uwanjani hawakuridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wa Stars ambapo baadhi yao walimlalamikia Kocha Marcio Maximo kwa kuchelewa kufanya mabadiliko kwani mshambuliaji Emmanuel Gabriel aliumia mapema lakini akalazimisha acheze dakika zote 45 za kipindi cha kwanza.

Mbali na mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Malawi, Stars pia inakabiliwa na kibarua cha kupambana na Sudan katika mechi ya mwisho ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani.

Katika mechi za raundi ya kwanza na ya pili, Stars iliitoa Timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars kwa mabao 2-1 kabla ya kuitoa Uganda, The Cranes kwa mabao 3-1 katika raundi ya pili.

Endapo Stars itaifunga Sudan, itafuzu fainali hizo za kwanza ambazo zimepangwa kufanyika mwakani nchini Ivory Coast.

Hata hivyo, Stars inatakiwa kujizatiti ili kuiondoa Sudan kwani imekuwa ikiisumbua mara kadhaa inapokutana nayo katika michuano mbalimbali inayohusisha nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Sudan ndiyo timu pekee kutoka Afrika Mashariki na Kati iliyofuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika zilizofanyika Januari mjini Accra, Ghana.

 

 

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents