Habari

Syria yaziba njia muhimu iliyokusudiwa kutumiwa na Uturuki, kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani kwazua mjadala

Vikosi vya serikali ya Syria vimeingia katika mji wa kimkakati wa Kobani, kuziba njia moja ambayo Uturuki iliazimia kuitumia, wakati hatua ya Trump kuondoa wanajeshi Syria ikileta mgongano Marekani.

Syrien Soldat der Armee in Tal Tamr (AFP/D. Souleiman)

Vikosi vitiifu kwa Rais wa Syria Bashar al-Assad vimeingia katika mji wa Kobani usiku wa kuamkia leo, hatua inayobadilisha hali ya mambo Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo. Mjini Kobani ndipo jeshi la Marekani lilipounda ushirika na wapiganaji wa Kikurdi katika vita dhidi ya Kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Kudhibiti mji huo kunaipa serikali ya rais Assad kuzuia mipango ya Uturuki kuunganisha maeneo madogo yaliyo chini ya uangalizi wale kaskazini magharibi mwa Syria, na mengine maogo iliyoyakamata kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wiki iliyopita, ili kuunda ukanda salama wenye upana wa km 30, kati ya mpaka wake na wapiganaji wa Kikurdi inaowachukulia kuwa magaidi.

Marekani yazidi kuihama miji ya Syria

Jana Jumatano Jeshi la Marekani lilitangaza kukihama kiwanda cha saruji kusini mwa Kobani, ambacho ilikitumia kama kituo cha uratibu wa ushirikiano wake na wapiganaji wa kikurdi.

Marekani pia iliipa kisogo miji mingine muhimu ya Raqqa na Tabqa, na msemaji wa ushirika wa kijeshi ilioongoza dhidi ya IS Kanali Myles Caggins, alisema kuwa wameziharibu shehena za silaha walizoziacha nyuma kwa kutumia ndege za kivita.

Mmoja wa makamanda wa jeshi la Syria Ahmad Hussein ameseme kuingia katika eneo hilo ni hatua muhimu kijeshi.

”Kituo cha jeshi la anga cha Tabqa ni muhimu kimkakati, kwa sababu kiko kaskazini mwa Syria. Kinachangia pakubwa katika kupeleka wanajeshi katika miji ya Hasakah, Aleppo na Raqqa, hadi mpakani kukabiliana na mashambulizi ya Uturuki”, alisema kamanda huyo.

Haya yanajiri wakati Rais wa Marekani akikabiliwa na ukosoaji unaozidi kuongezeka, kutokana na uamuzi wake wa kuwatupa mkono wapiganaji wa kikurdi waliopigana bega kwa bega na jeshi la Marekani kwa muda mrefu, katika mtindo ambao Wakurdi hao wameuita usaliti.

Azimio la kumlaani Trump lapita kwa kura nyingi bungeni

Baraza la Wawakilishi mjini Washington limepitisha kwa kura nyingi azimio la kuulaani uamuzi huo wa Rais Trump. Azimio hilo ambalo vile vile lilimtaka rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kusitisha mara moja mashambulizi kaskazini mwa Syria, lilipita kwa kura 354 dhidi ya 60 zilizolipinga. Wabunge 129 kutoka chama cha Republican cha Rais Trump waliungana na wademocrats katika azimio hilo.

Licha ya shinikizo hilo lakini, Donald Trump ameendelea kutetea uamuzi wake, akisema mzozo kwenye mpaka wa Uturuki na Syria unazihusu nchi hizo majirani, na wala sio Marekani. Hali kadhalika amebadilisha kauli yake ya siku chache zilizopita alipowasifu wapiganaji wa Kikurdi kama watu wema, kwa kusema wao pia wanayo makosa, na hawawezi kuchukuliwa kama malaika.

Sambamba na msimamo huo lakini utawala wa Trump unaendeleza juhudi za kuishinikiza Uturuki kusimamisha operesheni zake za kijeshi ndani ya Syria, na leo hii makamu wake Mike Pence na waziri wake wa mambo ya nje Mike Pompeo, wanatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais Erdogan wa Uturuki mjini Ankara kuhusu mzozo huo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents