Habari

Vurugu yazuka katika concert ya Alpha Blondy na Tarrus Riley nchini Kenya, baada ya wanamuziki hao kushindwa kutokea kwenye show!

Icon wa muziki wa Reggae Alpha Blondy kutoka Ivory Coast na Tarrus Riley kutoka Jamaica waliokuwa wanasubiriwa kwa hamu kutumbuiza katika viwanja vya KICC jijini Nairobi jana (June 15), walishindwa kutokea kwenye show kitendo kilichosababisha vurugu kutoka kwa mashabiki waliohudhuria kwa lengo la kuwashuhudia wanamuziki hao.
Tarrus na Alpha
Tarrus Riley (kushoto) na Alpha Blondy (kulia) wakati wanawasili Kenya

Kwa mujibu wa mtandao wa Ghafla wa Kenya, ratiba ya tukio ilikuwa inaonesha wanamuziki hao wangeanza kuzikonga nyoyo za mashabiki wao mishale ya saa 5 za usiku, lakini muda huo ulipofika hakuna cha Blondy wala Riley aliyeonekana si tu jukwaani bali hata katika eneo la tukio.

Yawezekana mwanzoni hakuna aliyejali sana sababu huwa kuna muda wa kila mtu kujipa majibu (huenda wamechelewa kufika tu) hivyo watu walikuwa wavumilivu, ukizingatia kwa wapenda burudani saa 5 usiku ni kama ndio muda wa kuamka ni mapema sana. Ilipofika saa 6 usiku siku na tarehe ikabadilika na kuwa (June 16) lakini bado hapakuwa na majibu jukwaani , hakuna Tarrus wala Alpha aliyekuwa amefika.

Tic Toc, tic toc…Mshale wa saa ukawa unazidi kusogea , mara saa 7 usiku, saa 8 subira ya mashabiki hao waliokuwa na kiu ya kuruka muziki wa Reggae ikaanza kuyeyuka na kuanza kuimba kwa pamoja “tunamtaka Tarrus, tunamtaka Tarrus”.

Baada ya saa nyingine moja kupita bila ya dalili za mastaa hao kuonekana ndipo sasa nguvu ya ziada ikaanza kutumika baada ya makopo ya soda kuanza kuvurumishwa jukwaani mithiri ya watoto wa primary wanapokutana na mti wa mapera yaliyoiva mchana wa saa 8 jua kali.

Waandaaji wa concert hiyo ‘Big Tunes’ walipoona vurugu imeanza walijaribu kuwatuliza watu hao bila mafanikio na badala yake vurugu iliendelea.
Ikiwa inaelekea asubuhi mida ya (3:30AM) watu walibadili nyenzo na kuanza kutupa chupa jukwaani kitendo ambacho kilipelekea waandaaji kuzima muziki kabisa na hapo ndio ghasia kubwa zikaanza.

Watu hao wenye hasira walianza kuharibu kila kitu walichohisi kinahusiana na waandaaji wakianzia na hema la ma DJ (DJ booth) ambayo waliharibu kila kifaa kilichokuwa kinatumika kupiga muziki katika tukio hilo na ma DJ ilibidi wakimbie ili kujiinusuru kuumizwa.

Wakati vurugu hizo zinaendelea watu hao walianza kupiga kelele za “Pombe, Pombe” huku wakielekea katika hema lililokuwa na vinywaji na chakula, unahisi nini kingine hapo kilifanyika zaidi ya kujichukulia makreti ya kila aina ya pombe na vyakula vilivyokuwa vinasubiri walaji.
Vurugu KICC

Mwandishi wa Ghafla aliyekuwepo eneo la tukio alilazimika kuficha camera yake ya kazi na kutumia simu kuchukua picha za matukio sababu yeyote aliyekuwa na professional camera kwaajili ya kazi pia alishambuliwa na watu hao wenye hasira.

Makopo wamesharusha, chupa wametumia, kilichofuata ni kuvunja viti ikiwa ni sehemu ya kuwapa hasara waandaaji kama waliyoipata wao kwa kulipa viingilio vya mpaka shilingi 5,000 ya Kenya kwa mtu mmoja ambayo ni karibia na laki 1 ya Tanzania.

Bado haijafahamika sababu zilizopelekea wanamuziki hao wa kimataifa kushindwa kutokea katika concert kubwa kama hiyo huku wote walikuwa wameshawasili Kenya. Tarrus Riley ndio alikuwa wa kwanza kuwasili Kenya Alhamisi (June 13) na kufuatiwa na Alpha Blondy aliyewasili Ijumaa (June 14).

Tazama video wakati MC wa shughuli alipokuwa anajaribu kuwatuliza watu

http://youtu.be/9sWgtEVBu2s

Source: Ghafla

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents