Habari

Wananchi kuulizwa kuhusu kunyongwa

SERIKALI inaandaa utaratibu wa kuwauliza wananchi iwapo sheria ya adhabu ya kifo iendelee kutumika au ifutwe.

Na Ramadhan Semtawa


SERIKALI inaandaa utaratibu wa kuwauliza wananchi iwapo sheria ya adhabu ya kifo iendelee kutumika au ifutwe.


Hatua ya ya serikali imekuja wakati tayari wanaharakati wa Haki za Binadamu nchini, wameonyesha kupinga adhabu hiyo na kutaka ifutwe.


Hoja ya msingi ya watetezi wa haki za binadamu nchini haitofautiani na wa kimataifa, ambao wanaona adhabu ya kifo kama inayoondoa haki ya kuishi kwa wanaokutwa na makosa na pia haitoa nafasi ya mtu kujirekebisha.


Hata hivyo, mchakato huo ambao haujaelezwa utaanza lini, utakwenda pamoja na elimu kwa wananchi kuhusu kuwepo kwa adhabu hiyo katika sheria za nchi kwa sasa.


Akizungumzia hatma ya adhabu hiyo juzi katika kipindi maalumu cha Bungeni Wiki Hii, kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TvT), Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Mary Nagu, alisema yeye binafsi anapinga adhabu ya kifo.


Hata hivyo, Dk Nagu alifafanua kwamba, kwa kuwa nchi inaendeshwa kwa mujibu wa katiba na sheria, hivyo kila mabadiliko yanapaswa kufuata vyombo hivyo.


“Binafsi, napinga adhabu ya kifo, lakini kama tunavyojua nchi hii inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na katiba,” alisema Dk Nagu na kuongeza:,


“Kwa hiyo serikali itaanda mchakato ili wananchi waamue kuhusu adhabu ya kifo, lakini kabla ya hapo watapaswa kupata elimu kuhusu adhabu hiyo,” alisisitiza.


Alisema wananchi lazima waelimishwe kuhusu sheria iliyounda adhabu hiyo ili hata wakitoa maoni, wawe na ufahamu wa jambo wanalochangia.


Katika hatua nyingine, Dk Nagu, alitetea uamuzi wa serikali ya CCM kuingiza katika ilani yake ya uchaguzi, suala la kutaka kupatia ufumbuzi wa Mahakama ya Kadhi nchini, akisema chama hicho hakikurupuka.


“Naomba niseme CCM haikukurupuka kuweka suala la kupatia ufumbuzi wa mahakama ya Kadhi katika ilani yake,” alisema Dk Nagu baada ya mbunge wa Karatu, Dk Wilbrod Slaa, kusema uamuzi huo wa chama hicho hicho tawala ni wa kukurupuka.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents