Habari

Vijana CCM wapigana kumrithi Amina Chifupa

BARAZA Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) limetaka nafasi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, marehemu Amina Chifupa, kupitia umoja huo, irithiwe na mtu kutoka Jumuiya hiyo.

na Martin Malera, Dodoma


BARAZA Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) limetaka nafasi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, marehemu Amina Chifupa, kupitia umoja huo, irithiwe na mtu kutoka Jumuiya hiyo.


Habari zilizoifikia Tanzania Daima Jumapili, kutoka ndani ya mkutano wa baraza hilo uliofanyika jana katika Ukumbi wa White House mjini hapa, zinaeleza kuwa wajumbe wengi walipinga utaratibu uliotumiwa na chama kumpata mrithi wa kiti hicho.


Habari hizo zinaeleza kuwa viongozi wakuu wa umoja walilazimika kufanya kazi ya ziada ya kutoa maelezo ya ziada kwa ajili ya kuwashawishi wajumbe ili kukubaliana na uamuzi wa chama wa kumpitisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Christine Ishengoma, kuwa mrithi wa kiti hicho.


Mkutano huo ambao ulifunguliwa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ulitawaliwa zaidi na mivutano ya hoja za wajumbe ambao walionyesha dhahiri kukerwa na kitendo cha kuteua mrithi wa nafasi hiyo kutoka Jumuiya ya Wanawake ya chama hicho (UWT).


Tayari jina la Dk. Ishengoma limekwisha kuthibitishwa na mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) uliomalizika hivi karibuni mjini hapa kuwa mrithi wa kiti cha Amina aliyefariki dunia Juni 26, na sasa linasubiriwa kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.


Habari zaidi kutoka ndani ya mkutano huo wa siku moja zilieleza kuwa hoja ya nafasi ya Amina Chifupa kuzibwa na mtu kutoka ndani ya Jumuiya hiyo, ilizua mjadala mkubwa ndani ya kikao hicho hadi Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dk. Emmanuel Mchimbi, kulazimika kutoa ufafanuzi juu ya taratibu za chama katika kuziba nafasi hiyo.


Baadhi ya wajumbe walioibua hoja hiyo kwenye mengineyo, walisema kuwa kwa vile Amina alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia UVCCM, ni bora nafasi hiyo ingejazwa na mtu mwingine ndani ya Jumuiya hiyo.


Kwa nyakati tofauti baadhi ya wajumbe wa mkutano huo walidai kuwa UVCCM katika uchaguzi uliopita, iliomba nafasi tano za viti maalumu, lakini chama kiliwapa viti viwili vilivyokuwa vikiwaniwa na Amina Chifupa, Lucy Mayenga na Vicky Kamata.


Hata hivyo Chifupa na Mayenga ndio walioibuka washindi na Kamata ambaye pia ni mwanahabari na mwanamuziki wa miondoko ya Zouk, kuachwa nje. Chifupa alikuwa mwanahabari, kama ilivyo kwa Mayenga.


Akitoa ufafanuzi wa suala hilo, Dk. Nchimbi alisema kuwa suala la Viti Maalumu liko ndani ya chama, hivyo si lazima mbunge wa Viti Maalumu anayetokea kwenye kundi lolote anapofariki, kufukuzwa au kuacha uwakilishi huo, mrithi wake atoke ndani ya kundi hilo.


Kwa mujibu wa habari hizo, Dk. Nchimbi alitolea mfano wa nafasi ya Dk. Asha-Rose Mtengeti Mingiro, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), kwamba alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Vyuo Vikuu, lakini aliyejaza nafasi yake, Florence Kyendesya, hakutoka katika kundi hilo.


Hata hivyo habari hizo zilieleza kuwa UVCCM imetaka suala la viti maalumu litenganishwe ili kama kuna nafasi imeachwa wazi kwa sababu zozote zile, mrithi wake atoke ndani ya jumuiya husika.


Wakati huo huo, Halmashauri Kuu ya CCM, NEC imewalaumu wabunge wa chama hicho, kuwa wamekuwa bubu katika vikao vya Bunge kwa kuogopa kuibana na Serikali, na badala yake kazi hiyo sasa imeachwa ifanywe na wabunge wa upinzani.


Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya NEC ambayo ilimaliza kikao chake juzi mjini Dodoma, zilieleza kuwa NEC haifurahishwi na jinsi wabunge wa CCM walivyo mabubu na jinsi wanavyoogopa kuikosoa serikali, kazi ambayo sasa inafanywa kwa ufanisi mkubwa na wabunge wa kambi ya upinzani.


Walisema hali hiyo ni hatari kwa chama kwani siku zijazo wananchi wanaweza kukosa imani na wabunge wa CCM na kuwachagua wapinzani.


Akifungua mkutano wa vijana jana, Lowassa aliwataka kuwa makini na matumizi ya dawa za kulevya na kujitokeza kuwania nafasi za uongozi kwa vile wana nafasi kubwa katika ujenzi wa taifa.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents