Habari

Hali tete Ulanga, Mbunge aeleza athari za kutisha za mafuriko

Amwangukia Rais Samia

WAKATI watoto saba wamepoteza maisha na zaidi ya kaya 70 kukosa makazi wilayani Ulanga, Mkoani Morogoro kutokana na athali za mafuriko, Mbunge wa Ulanga Mashariki, Salim Alaudin Hasham (CCM), ameeleza athari za kutisha.

Mbunge huyo amemwangukia Rais Samia Suluhu Hassan kunusuru hali hiyo kwani wilaya ya Ulanga haina mawasiliano na gharama za maisha zimepanda mara dufu.

Mbunge huyo amebainisha hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Morogoro juu ya athali za mafuriko yaliyowakumba wakazi wa jimbo lake na kusisitiza kuwa hali ni mbaya kwa sasa na waathirika wanahitaji msaada wa dharula.

Salim ametaja athali nyingine kuwa ni pamoja na wananchi kupoteza heka elfu tano(5,000) za mazao yaliyokuwa shambani na kuwaacha wananchi wengi wakiwa hawana chakula hali iliyomlazimu kupaza sauti kwa Seikali na wadau wengine kuangalia namna ya kuwanusuru waathilika hao wa mafuriko.

Akizungumzia hali ya Miundombinu ya barabara Mbunge wa jimbo la Ulanga amewaambia waandishi wa habari kuwa kwa sasa mawasiliano ya barabara ya Lupiro – Mahenge yamekatika na kusababisha adha kubwa ya usafiri kwa kuwa hakuna magari yanayoweza kuingia na kutoka katika mji wa Mahenge ambao ni makao makuu ya wilaya.

Amesema kulingana na adha hiyo gharama ya maisha imepanda mara dufu kwani kutokana na wafanyabiashara kufikisha bidhaa hiyo kwa ugumu zaidi, huku akibainisha kuwa kwa sasa kilo moja ya chumvi iliyokuwa inauzwa shilingi mia 500 sasa inauzwa shilingi elfu 2,000, Sukari imepanda na kufikia shilingi 7,000, wakati unga ukiuzwa kwa zaidi ya shilingi 3200, gharama ambayo wananchi walio wengi hawawezi kuimudu.

Salim amesema gharama za maisha zimepanda zaidi kutokana na miundombinu ya barabara kuharibika na kusababisha magari kushindwa kufanya safari za kuingia na kutoka Mkao makuu ya wilaya ya Ulanga, huku akieleza kusikitishwa na ukimya wa Wakala wa Barabara Tanroads licha ya kufikishiwa changamoto iliyopo kwa zaidi ya miezi minne sasa.

“Hatuwezi kuilaumu Serikali au chama cha Mapinduzi, kwa uzembe unaofanywa na watendaji waliopewa mamlaka ya kufanya hizo shughuli na kushindwa kutimiza wajibu wao kwa kisingizio cha mvua” alisema Mbunge

Kiongozi huyo wa jimbo la Ulanga pia amekanusha uvumi kuwa Tanroads walimpiga faini, baada ya yeye binafsi kuamua kurekebisha baadhi ya maeneo yaliyoharibika akisisitiza kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowowte bali zinapotoshwa na baadhi ya watu wasio na mapenzi mema kwa wana Ulanga wanaotamani kuona wananchi wanaendelea kutaabika.

Katika Hatua nyingine Mbunge alisema licha ya mvua kuendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali lakini kinachosikitisha zaidi ni kuona hakuna hata kiongozi mkubwa aliyefika kuwafariji wananchi wa Ulanga hali inayowafanya wananchi kujihisi kuwa wametengwa na Serikali yao na kujiona kuwa siyo sehemu ya Wanzania.

“Tunaamini kuwa hali ya mvua inaendelea nchi nzima na inawezekana tusipate msaada wa haraka kutokana na hali inayoendelea, lakini hatuhitaji mje mtusaidie lakini Serikali tunahitaji tupate faraja wananchi wa jimbo la ulanga wanahitahi faraja, sasa taarifa zinaenda kwa Mawaziri, zinafika kila Sehemu tunaona jinzi ambavyo Mawaziri wanatembea kila Sehemu kwenda kuangalia adha inayowakuta wananchi katika maeneo yao, lakini jimbo la ulanga limekuwa kama siyo Tanzania inafika wakati wananchi wa Ulanga Wananiuliza kwamba labda sisi siyo Watanzania labda sisi Rais wetu siyo Mama Samia Suluhu Hassani?” alisema Mbunge Salim

Alisema amelazimika kuzungumza na Vyombo vya habari ili Rais Dkt Samia Suluhu Hassani licha ya kuwa kipenzi cha wananchi wote lakini ajue ni aina gani ya watendaji anaowaajiri namna wanavyo muangusha katika kuwatetea wananchi wanyonge

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents