Habari

Waziri Mkuu aagiza maofisa 4 wawekwe rumande

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji awakamate maofisa wanne na kuhakikisha wanapelekwa wilayani Masasi mkoani Mtwara chini ya ulinzi ili wajibu tuhuma za upotevu wa tani 2,138 za korosho.

Kufuatia agizo hilo, Polisi imewatia mbaroni watuhumiwa hao na juzi walipandishwa katika gari la jeshi hilo na kupelekwa Masasi.

Maofisa hao ni Kaimu Meneja Mkuu Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi (MAMCU), Kelvin Rajab na Meneja Tawi wa MAMCU, Lawrence Njozi,wakurugenzi wa kampuni ya YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa mazao kwenye maghala, Yusuph Namkukula na Ramadhani Namakweto.

Majaliwa alifikia uamuzi huo juzi jioni kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini baina ya watendaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, MAMCU, wamiliki wa ghala la BUCO-Masasi na kikundi cha wakulima sita waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya msingi (AMCOS) za wilaya za Mtwara na Masasi.

Katika kikao hicho, Majaliwa alitaka maelezo ya kina ni wapi zilipo tani 2,138 za korosho wakati taarifa waliyompa viongozi hao ilionesha waliuza korosho na hakuna hata kilo moja ambayo haijanunuliwa katika mnada wa tano uliofanyika Novemba 10, mwaka jana.

Kaimu Meneja Mkuu wa MAMCU, Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba korosho zote ziliuzwa na zilishalipwa na wanunuzi wa mnada wa tano lakini akadai hakupewa taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha korosho. Naye mmiliki wa ghala la BUCO, Ramadhan Namakweto alikiri kupokelewa kwa korosho hizo ghalani kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni kwa nini hazionekani zilipo.

“Haiingii akilini mnada wa mwezi wa 11,korosho zinakuwa ndani ya ghala minada mingine inakuja, korosho zinakuja leo zinauzwa za juzi zinaachwa, toka mwezi wa 11 mpaka mwezi wa 1 mwaka 2017 haiwezekani, kama yuko wapi utaondoka na hawa wa maghala wawili na wa MAMCU wawili hawa warudishwe Masasi kwa ulinzi wakajibu tuhuma zifuatazo kwa kuzificha korosho tani 2,138 na wamezihifadhi kwenye ghala humo kutoka tarehe 11 mwezi wa 11 hawajaziuza mpaka leo,tunataka tujue kwanini korosho hizo zilikuwa haziingii mnadani,” aliagiza Majaliwa.

Aidha Waziri Mkuu pia alimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa hesabu za MAMCU na kujiridhisha kiasi cha korosho kilichonunuliwa; fedha zilizolipwa na kuingia akaunti za MAMCU; kiasi cha fedha zilizolipwa kwa vyama vya msingi na wananchi kwa ulinganifu na bei ya korosho kwa kila mnada husika.

BY: Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents