1,700 wa vijiji vinne Kisarawe waamriwa kuhama

Zaidi ya wakazi 1,700 wa vijiji vinne katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, hawana mahali pa kuishi baada ya kuamriwa kuhama makazi wanayoishi.

Na Richard Makore



Zaidi ya wakazi 1,700 wa vijiji vinne katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, hawana mahali pa kuishi baada ya kuamriwa kuhama makazi wanayoishi.


Wakazi hao wamedai kuwa wamekuwa wakiishi katika maeneo hayo tangu mwaka 1976.


Agizo la kuondoka kwa wananchi hao lilitolewa na uongozi wa 83 KJ kilichopo wilayani humo.


Kufuatia agizo hilo, hivi sasa baadhi ya wananchi hao wameanza kufunga virago na kuondoka.


Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wananchi hao walidai kuwa, amri hiyo ilitolewa Ijumaa iliyopita na kwamba hivi sasa wanaishi katika wasiwasi mkubwa.


Wananchi walioamriwa kuhama wanatoka katika vijiji vya Tondoloni, Kwembe, Kiluvya B na Mloganzila.


Mwenyekiti wa kamati ya kudai haki za wananchi hao, Bw. Chris Baijuka, alisema kikosi hicho kiliwakuta wananchi hao wakiishi hapo tangu mwaka 1979 kilipoanzishwa.


Alisema mwaka 1986, kikosi hicho kiliomba kupanua eneo hilo kwa ajili ya kufanyia mazoezi lakini kwa makubaliano kwamba wawalipe fidia.


Aliongeza kuwa, jukumu hilo la kuwalipa lilichukuliwa na Wilaya ya Kisarawe lakini halikutekelezwa ipasavyo.


Alifafanua kuwa, kila mwananchi alkiyetakiwa kulipwa alipewa bahasha lakini hakuruhusiwa kufungua pale pale mpaka afike nyumbani.


Alidai kuwa, vijiji vinavyodaiwa kuwa ni eneo la jeshi vilisajiliwa na serikali tena kwa mujibu wa sheria na vinatambuliwa.


Bw. Baijuka alisema, kinachowaogopesha ni kauli za vitisho zinazotolewa na wanajeshi hao kila wanapopita kijijini kwao.


Alimshutumu Mwenyekiti wa kijiji cha Mloganzila, Bw. Mohamed Kikonyo, kwa madai kuwa anawasaliti wenzake na kuwatetea wanajeshi.


Naye mkazi mwingine wa kijiji cha Mlaoganzila, Bi. Asha Shomari (80), alisema kitendo kinachofanywa na wanajeshi hao ni ukatili kwani yeye alianza kuishi hapo tangu akiwa msichana na hajawahi kulipwa fidia wala kuambiwa hatakiwi kukaa hapo.


Alisema katika jambo hilo, lazima serikali iingilie kati kwani na wao ni Watanzania sawa na wengine hivyo wanahitaji haki ya kulindwa wao na mali zao.


Alisema mwaka 1986 Wilaya ya Kisarawe ilitangaza kuwalipa fidia lakini walipokwenda wengine waliambulia Sh. 2,000 zikiwa ndani ya habasha ambapo wengi wao walizikataa.


Alifafanua kuwa, wananchi wengi walipofika njiani na wengine nyumbani, walichokikuta hawakuamini.


Akizungumza na Nipashe, Mjumbe wa shina wa CCM, Bw. Richard Mng`ong`ose alisema, anawashangaa viongozi wa serikali kwa kukaa kimya juu ya jambo hilo wakati wao ni wapiga kura wao.


Alisema kipindi cha uchaguzi kikifika wanawathamini na kuwapenda lakini baada ya kupata kura wanawaona kama takataka na hakuna mtu aliyefika hapo kuwaona.


Alisema kesho ndiyo siku ya mwisho waliyopewa na wanajeshi hao na waliambiwa wasipoondoka wataondolewa kwa nguvu, kubomolewa nyumba zao pamoja na kuharibiwa mali.


Alisema wanachi hao wamepewa barua yenye kumbukumbu namba 83 regt/2153-1. kutoka kikosi cha 83 KJ inayowataka kuhama mara moja ifikapo kesho.


Nakala ya barua hiyo ambayo Nipashe inayo imesambazwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mkurugenzi wa Wilaya, Ofisa Ardhi wa Wilaya na Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mloganzila.


Wananchi hao walidai kuwa wameandika barua kwa Waziri Mkuu, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, TAMISEMI lakini hawajapata jibu lolote.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents