Habari

Askofu anayeshikiliwa mahabusu kwa zaidi ya miezi tisa sasa aibua mapya

Askofu anayeshikiliwa mahabusu kwa zaidi ya miezi tisa sasa aibua mapya

ASKOFU Mulilege Kameka anayeshikiliwa mahabusu kwa zaidi ya miezi tisa sasa kwa tuhuma za kutokuwa raia wa Tanzania, ameibuka na mpya akiomba Mahakama Kuu  iwatie hatiani Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Uhamiaji. Kameka ambaye ni Askofu wa Kanisa la House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship (HPSFCFC), ameleta maombi hayo huku akiiomba mahakama hiyo iwahukumu kifungo kwa kudharau amri ya mahakama.

Maombi hayo yaliyofunguliwa Julai 16, mwaka huu, yalipangwa kusikilizwa jana na Jaji Atuganile Ngwala.

Hata hivyo, upande wa Serikali ambao ni wajibu maombi hayo, waliwasilisha pingamizi la awali.

Baada ya pingamizi hilo, mahakama hiyo imepanga Agosti 9, mwaka huu, kutoa uamuzi juu ya pingamizi lililowasilishwa na upande wa Serikali dhidi ya maombi hayo. Uamuzi huo wa mahakama unatarajiwa kutolewa na Jaji Ngwala, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili kuhusu pingamizi hilo.

Katika pingamizi hilo, upande wa Serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi ,Jackline Nyantori, ulidai kuwa kifungu cha sheria ambacho wapeleka maombi wamekitumia, hakiipi mamlaka Mahakama Kuu kusikiliza maombi hayo. Upande huo ulisisitiza kuwa kosa linalodaiwa kutendeka halikufanyika mbele ya mahakama, hivyo waombaji walipaswa kupeleke malalamiko hayo kwanza polisi na kuleta madai, ndipo mahakama iyasikilize na kuyatolea uamuzi.

Akijibu hoja hiyo, wakili wa mpeleka maombi, John Mallya, alidai kuwa maombi hayo yameletwa kwa taratibu na kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa Mtanzania Digital. Aliongeza kuwa sheria inaruhusu kuleta maombi ya aina hiyo kwa njia ya hati ya maombi na kiapo kama walivyofanya.

Machi 18, mwaka huu, mahakama hiyo iliamuru askofu  huyo aliyekuwa akishikiliwa akidaiwa kuwa si raia wa Tanzania aachiwe huru kwani uraia wake hauna shaka na kama kuna pingamizi litolewe ndani ya saa 48.

Amri hiyo ilitolewa na Jaji IIvin Mgeta ambaye alitoa maelekezo kuwa askofu huyo atolewe mahali anaposhikiliwa kwani vilelezo vilivyotolewa vimethibitisha uraia wake kuwa ni Mtanzania. Licha ya amri hiyo kutolewa, hadi leo bado askofu huyo anashikiliwa na yuko mahabusu gerezani.

Chanzo Mtanzani:- https://mtanzania.co.tz/askofu-anayeshikiliwa-mahabusu-aibua-mapya/

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents