Habari

Prof Lipumba adai kuwa yeye bado ni mwenyekiti halali wa CUF

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Prof Ibrahim Lipumba amesema yeye ndiye mwenyekiti halali wa chama hicho licha ya Baraza Kuu la chama hicho kutangaza kumsimamisha uanachama, yeye na wenzake 10.

Profesa-Ibrahim-Lipumba-640x559

Lipumba akiongea na kituo cha ITV amesema kikao kilichokaa jana visiwani Zanzibar na kufanya maamuzi ya kuwasimamisha uanachama, hakikuwa halali na kilikuwa nje ya katiba ya CUF, sababu mojawapo ikiwa ni kuwekwa kando kwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya.

“Hicho kikao hakikuwa halali, haiwezekani Baraza Kuu linakaa halafu Naibu Katibuy Mkuu Bara hajui, wala hakujulishwa, na bado kuna wajumbe wengine hawakuhusishwa” Amesema Prof Lipumba

Lipumba amesema ni kweli alijiuzulu uenyekiti, lakini baadaye aliamua kuandika barua kwa Katibu Mkuu ya kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu na sasa yeye ndiye Mwenyekiti wa chama hicho.

“Nilimuandikia barua ya kurudi kwenye nafasi yangu, akasema anasubiri ushauri wa kisheria, lakini hadi sasa hakuna kitu, hiyo inamaanisha kuwa sasa mimi naendelea na nafasi yangu, na niko ngangari kama mwenyekiti” Amesema Prof Lipumba.

Amesema alitaka kujieleza katika mkutano mkuu mbele ya wanachama, lakini mkutano ule ukavurugwa.

Kuhusu kuwepo kwa tofauti kati yake na Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, Prof Lipumba amesema kuwa huenda kuna tofauti kwa kuwa mara nyingi huwa hamuelewi jinsi anavyokiendesha chama bila kifuata misingi ya kidemokrasia.

“Katibu Mkuu anamdharau na hampi heshima yake Naibu Katibu Mkuu Bara, mara nyingi huamua mambo yake bila kushirikisha viongozi wengine, halafu sasa anataka kufukuza wanachama, huwezi kuwa na chama halafu ufukuze wanachama, wanachama wanatafutwa duniani kote, halafu wewe unawafukuza, hizo ni dalili za uongozi wa kiimla, kuongoza chama unapaswa kujali demokrasia na siyo kuwa dikteta ndani ya chama” Amesema

Kuhusu Julius Mtatiro kuwa mwenyekiti mpya wa Kamati ya Uongozi, Lipumba amesema kuwa hatambui maamuzi hayo, na wala hamtambui Mtatiro kama kiongozi wa chama hicho bali mjumbe wa Mkutano Mkuu, nafasi ambayo yeye ndiye aliyempa.

“Mtatiro hawezi kuwa mwenyekiti, mimi ndiye mwenyekiti wa chama, Mtatiro alishindwa hata kuongoza mkutano mkuu, ukavurugika, hawezi, simtambui”

Source: eatv.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents