Bei za vyakula zapanda tena

PAMOJA na kauli ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustapha Mkulo kuwa pato la Taifa limeongezeka na kuchangia kukua pato la wastani wa Mtanzania mmoja mmoja kati ya mwaka 1992 na mwaka huu, hali ya maisha ya Watanzania inazidi kuwa taabani

Na Eben-Ezery Mende




PAMOJA na kauli ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustapha Mkulo kuwa pato la Taifa limeongezeka na kuchangia kukua pato la wastani wa Mtanzania mmoja mmoja kati ya mwaka 1992 na mwaka huu, hali ya maisha ya Watanzania inazidi kuwa taabani kutokana na kupanda kila siku bei za bidhaa madukani hususani vyakula na kutishia kutimia ndoto za Maisha Bora kwa kila Mtanzania.

Mapema wiki hii, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Bw. Mkulo alitoa takwimu zikionesha ukuaji mzuri wa pato la Taifa ambapo alisema mwaka 2007 pato hilo lilikuwa sh. trilioni 18 na mwaka huu linatarajiwa kufikia sh. trilioni 25.

Alisema kutokana na ukuaji huo, pato la Mtanzania mmoja mmoja nalo limeongezeka kutoka sh. 480,000 mwaka 1992 hadi sh. 545,455 mwaka 2007 na linatarajia kufikia sh. 631,300 mwaka huu.

Hata hivyo,Bw. Mkulo katika takwimu zake alishindwa kutoa takwimu zinazoonesha pengo lililopo sasa kati ya wenye nacho na wasionacho na kukiri kuwa serikali haijafanya utafiti unaoweza kutoa takwimu hizo.

Wakati Bw. Mkulo akitamba kukua kwa pato la Taifa sambamba na la Mtanzania mmoja mmoja, bei za vyakula madukani na katika masoko mbalimbali zimekuwa zikipanda siku hadi hali inayowafanya mamilioni ya Watanzania kukuza mkanda ambao sasa unakaribia ‘kugusa mifupa.’

Jijini Dar es Salaam imeelezwa kuwa bei za vyakula zimepanda kwa zaidi ya asilimia 12 ikilinganisha na mwanzoni mwa mwaka huu.

Ongezeko hilo limeibua ‘kilio’ kwa wananchi wengi hususani wa kipato cha chini ambao sasa wameshuhudia kupanda mara dufu kwa bei za ‘bidhaa wakombozi’ kama chumvi na maharage ambazo kwa muda mrefu hawakuwahi kushuhudia ongezeko la bei zake.

Uchunguzi uliofanywa na Majira katika maduka mbalimbali jijini umebaini kuwa sukari ambayo mwanzoni mwa mwaka iliuzwa sh. 950 kwa kilo, sasa imefikia sh. 1,200 unga wa ngano umepanda kutoka sh. 750 kwa kilo na kufikia sh. 900. Sembe imepanda kutoka sh. 550 na kufikia sh. 700. Mafuta ya kupikia (Korie) ujazo wa lita 20 yamepanda kutoka sh.38,000 na kufikia sh. 44,000.

Mche wa sabuni ya kufulia ambao awali uliuzwa sh. 750 sasa umefikia sh. 1,000, kiberiti nacho kimepanda kutoka sh. 40 hadi sh. 50, mshumaa sasa unauzwa sh. 150 badala ya sh. 100, sabuni ya kufulia ya unga yenye ujazo wa gramu 50 awali iliuzwa sh. 150 sasa imefikia sh. 200.

Mkate wa gramu 500 mwanzoni mwa mwaka uliuzwa sh. 450 sasa unauzwa sh. 600, majani ya chai paketi ya gramu tatu awali iliuzwa sh. 10 sasa ni sh. 25, lita moja ya mafuta ya taa imepanda kutoka sh. 970 na kufikia sh. 1,300

Gunia la mkaa mwanzoni mwa mwaka lililouzwa sh. 19,000 sasa limefikia sh. 30,000. Nyama ya ng’ombe (steki) imepanda kutoka sh. 3,000 kwa kilo hadi sh. 4,000 na mchanganyiko kutoka sh. 2,500 hadi sh.3,000. Chumvi ya ujazo wa gramu 200 awali iliuzwa sh. 100 sasa imefikia sh. 150

Mchele wa Mbeya sasa umefikia sh. 1,500 kwa kilo huku maharage (soya) yakigota sh. 1,600. Awali katika masoko ya Dar es Salaam hususan Tandale soya iliuzwa sh. 1,000. Vyakula vingine mfano viazi mviringo vimepanda kutoka sh. 20,000 kwa gunia na kufikia sh. 30,000

Mkungu wa ndizi aina ya mshale awali uliuzwa sh. 6,300 sasa umefikia sh. 15,000, wakati malindi umepanda kutoka sh. 7,000 na kufikia sh. 13,000.

“Bei ya vyakula zilianza kupanda zaidi mwanzoni mwa mwaka huu hasa pale bei ya mafuta ilipopanda, “alisema Bw. Ally Uledy mmoja wa viongozi katika Soko la Tandale, jijini Dar es Salaam .

Akielezea upatikanaji wa vyakula hivyo mikoani, mmoja wa wafanya biashara wa mchele wa Mbeya sokoni hapo, Bw. Suleman Said, alisema kuna uhaba mkubwa wa chakula hicho kutokana na msimu wa mavuno unaoendelea.

“Mimi nafanya biashara ya mchele kwa miaka mitano sasa, upandaji bei wa mwaka huu umekuwa mkubwa sana kutokana na mambo mengi, kwanza ni kupanda kwa bei ya mafuta, ukame kwa baadhi ya mikoa na baadhi ya wakulima kukata tamaa kutokana na kupata hasara msimu wa mwaka jana,” alisema.

Mbali na kupanda bei za vyakula, bidhaa zingine kama vifaa vya ujenzi nazo zimepanda bei mara dufu wakati saruji iliyokuwa ikiuzwa kati ya sh. 11,500 hadi 12,500 mwanzoni mwa mwaka sasa inauzwa kati ya sh.15,500 na sh. 16,500.

Wakati bei hizo zikipanda zipo taarifa za ongezeko la bei ya mafuta kwenye soko la dunia hali inayotishia kuzidi kupanda zaidi kwa bei za bidhaa zingine.

Takwimu zinaonesha kuwa pipa la mafuta ghafi sasa limefikia dola za Marekani 120 na hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu linatarajiwa kufikia dola 200. Januari pipa liliuzwa kwa dola 60.


 


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents