Corona Afrika Kusini bado kitendawili, ongezeko kubwa la maambukizi shule zafungwa kwa wiki nne

Afrika Kusini imefunga shule kwa wiki nne kuanzia Jumatatu kama sehemu ya kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona. Rais Cyril Ramaphosa amesema ilikuwa muhimu kuhakikisha shule hazigeuki kuwa vituo vya maambukizi wakati ambapo idadi ya wanaoathirika nchini humo inazidi kuongezeka kwa kasi ya juu mno duniani.

Shule za msingi na sekondari zilifunguliwa tena Julai 6.

“Kwa kuzingatia maoni ya washikadau na wataalamu mbalimbali, baraza la mawaziri limeamua kwamba shule zote za umma zitachukua mapumziko ya wiki nne,” amesema Rais Ramaphosa. Alisema kuwa mwaka wa sasa wa masomo utaongezwa hadi zaidi ya 2020 kwa sababu ya janga la corona.

“Tumechukua njia ya tahadhari kufunga shule kipindi hiki ambapo nchi inatarajiwa kupata maambukizi ya juu zaidi,” alisema. Aidha, rais pia ametangaza mfuko wa fedha wa dola bilioni 30 sawa na pauni bilioni 24 kufadhili huduma za afya na kusaidia wenye uhitaji zaidi.

Idadi ya wanaokufa huenda ikawa juu zaidi ya inayotangazwa Watafiti Afrika Kusini wanasema kuwa idadi ya waliokufa kwa virusi vya corona huenda ikawa ni ya juu zaidi kuliko takwimu rasmi zinazotolewa na serikali.

Baraza la Utafiti wa Matibabu Afrika Kusini limesema kwamba idadi ya wanaokufa iliongezeka kwa 17,000, asilimia 59 zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Profesa Debbie Bradshaw, mmoja wa waadhishi, amesema wamegundua tofauti kubwa ya idadi ya wanaokufa inayotolewa. Alhamisi nchi hiyo ilithibitisha vifo 572 kwa kipindi cha saa 24. Sasa hivi, Afrika Kusini ni ya tano kwa idadi ya waliothibitishwa kupata maambukizi duniani ikiwa na zaidi ya maambukizi 400,000 na vifo 5,940.

Ripoti hiyo inasemaje?

Ripoti iliyotolewa na Baraza la Utafiti wa Matibabu Afrika Kusini inaonesha kuwa kati ya Mei 6 na Julai 14 mwaka huu kulikuwa na vifo 17,090 vilivyotokea kwa njia ya asili – idadi hiyo ikiwa ni ya juu zaidi ikilinganishwa na miaka iliyotangulia hata kuliko vile watafiti walivyokuwa wametabiri.

Pia haijafahamika ikiwa idadi ya sasa ya juu ya vifo inayorekodiwa inahusiana moja kwa moja na virusi vya corona lakini watafiti wanafikiri kuwa huenda ikawa miongoni mwa sababu. Pia kuna wasiwasi kwamba watu wanakufa kwasababu hawapo karibu na hospitali, kwa hofu ya kupata maambukizi au kwasababu ya ukosefu wa nafasi ya kujitenga.

Rais wa Baraza hilo Profesa Glenda Gray alisema ongezeko hilo huenda kunatokana na ugonjwa wa Covid-19 au hata magonjwa mengine kama vile kufua kikuu, Ukimwi na hata magonjwa yasioweza kuambukiza”.

Je Afrika Kusini imeshughulikia vipi janga hili?

Afrika Kusini ni nchi ambayo imeathirika vibaya na virusi vya corona. Rais Ramaphosa aliweka hatua kali za kukabiliana na janga hilo mwisho wa Mei, ikiwemo hata kuuza sigara na pombe ili kupunguza shinikizo kwa wahudumu wa afya.Hatua hizo zilitekelezwa na maafisa wa jeshi waliosambazwa mitaani ili kuweza kudhibiti ugonjwa wa virusi vya corona.

Mamlaka baadae iliondoa marufuku ya kuuza pombe wakati ambapo shughuli za kibiashara zilikuwa zimeanza tena na watu kurejea kazini Lakini siku za hivi karibuni maambukizi yamekuwa yakiongezeka.

Hata h ivyo, Rais Ramaphosa alirejesha tena marufuku ya kuuza pombe Julai nchi hiyo ilipokuwa inakabiliana na ukosefu wa vitanda hospitalini. Hadi kufikia sasa idadi iliyothibitishwa kwa waliopata maambukizi ya virusi vya corona inaongezeka kwa zaidi ya 10,000 kwa siku.

Related Articles

Back to top button