Burudani

D’Banj na Yaya Toure waunga mkono kampeni ya kilimo ya Rais Kikwete

Msanii wa muziki kutoka Nigeria D’Banj pamoja na mchezaji wa Manchester City,na timu ya Taifa Ivory Coast Yaya Toure, wameiunga kampeni inayohamasisha vita dhidi ya umaskini kwa kutumia kilimo iliyoasisiwa na Rais Jakaya Kikwete na Shirika la One la Marekani.

page

D’Banj alishirikiana na washirika wa Kilimo wa Afrika katika uzinduzi wa kampeni ya ‘Shiriki Kilimo’ (Do Agric) kwenye kongamano la Umoja wa Afrika. Kampeni hiyo inalenga kuwasaidia watu zaidi ya milioni 85 barani Afrika kutoka katika lindi la umasikini kupitia uwekezaji maalumu katika kilimo na sera za kilimo za Maputo zilizoboreshwa.

D’Banj alikuwa mmoja wa waliozungumza Addis Ababa jana wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo yenye lengo la kuwahamasisha viongozi wa kisiasa kutumia sera nzuri zitakazonyanyua uzalishaji, kuongeza kipato na kuondoa mamilioni ya Waafrika kutoka katika umasikini.

“Nataka Waafrika kufahamu kilimo ni msingi mzuri wa uchumi ambacho kinatakiwa kutiliwa mkazo na kuleta mabadiliko katika uchumi wa wananchi na nchi na pia tukitilia mkazo tunaweza kuilisha dunia nzima kwa ujumla sisi kama Waafrika,” alisema D’Banj.

Kwa upande wake mchezaji wa timu ya Manchester City, Toure alisema wakati viongozi wengine wa Kiafrika wakitoa kauli zenye nia njema, kwa sasa ni nchi 8 tu zililizotimiza ahadi zake za kuwekeza 10% ya bajeti za nchi katika kilimo.

“Kwahiyo ni muhimu kufanya zaidi na kwenda mbele zaidi. Kilimo sio muhimu pekee, pia ni lazima. Kilimo kinalipa,” alisemaToure.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na asasi mbalimbali za kiraia zikiwemo Pan African Farmers Association (PAFO), Action Aid International , Acord International, Oxfam na Alliance for Green Revolution In Africa (AGRA) mbali na asasi hizo mwanasoka wa kimataifa wa Ivory Coast Yaya Toure pia ametia saini kuunga mkono uhamasishaji huo.

Source:Habari leo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents