Habari

Dkt. Bashiru Ally arithi mikoba ya Kinana CCM

Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi(CCM) imempitisha Dkt. Bashiru Ally kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Abdulrahman Kinana.

Rais Magufuli akiwa na Katibu Mkuu mpya wa CCM, Dkt. Bashiru Ally

Dkt. Bashiru ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Tume maalum ya kuchunguza mali za CCM iliyoundwa na Rais Magufuli.

Aidha Raymond Mangwala ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) ndani ya chama hicho tawala katika mkutano wa siku mbili uliomalizika jijini Dar es Salaam.

Siku ya Jumatatu CCM kilipokea barua ya kustaafu ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho tawala Abdulrahman Kinana.

Akiongea katika kikao hicho, mwenyekiti wa chama cha CCM rais wa Tanzania John Magufuli amepongeza kazi iliyotokana na tume iliyokuwa chini ya uongozi wa Dkt Bashiru iliyoshughulika na uhakiki wa mali za chama na kusema kwamba anatumai kuwa katibu mkuu huyo mpya atatumia aliyoyaona katika kukiendeleza chama katika wadhifa huo mpya.

‘Tumekupa jukumu hili tukiwa na matumaini makubwa kwamba yote uliyoyaona kwa miezi mitano sasa ukayafanyie kazi katika Chama chote na jumuia zake kwa nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM’, amesema Rais Magufuli.

Kuondoka kwa Kinana ndani ya Chama kulizua maswali kuhusiana na nani ataweza kuvaa viatu vyake, na hasa baada ya kurejea kazi alizozifanya za kisiasa kwani Kinana aliongoza kampeni za rais wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa, na kusimamia kazi mbali mbali za utekelezaji wa ilani ya chama hicho.

Falsafa yake ya kijamaa, imejenga wasifu wa nje wa Kinana unaoakisi kusimamia kile alichokiamini ndani ya chama chake,huku akitajwa kubobea katika uenezi na ambaye amepata mafunzo katika nchi mbali mbali za kikomunisti jambo ambalo linazidisha kuendelea kuhitajika kwake hata alipoamua kustaafu.

Hata hivyo katika shughuli za ujenzi wa chama akiwa katibu mkuu wa chama , Kinana alizunguka nchi nzima kufanya shughuli mbali mbali za chama akishirikiana na watu katika kazi za mikono na kula nao chakula jambo ambalo linatajwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa kwamba lilikiimarisha zaidi chama hicho na kuongeza mshikamano.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents