Burudani

Exclusive: Meninah asimulia jinsi alivyolazimika kulipa gharama za kununua gari jipya baada ya kuunguza gari akishoot video Kenya

Muimbaji wa kundi la Shosteez, Meninah Atick, amesema alilazimika kulipa gharama za kununua gari jipya baada ya kuunguza kwa moto gari lililokuwa limeegeshwa jirani na eneo walilokuwa wakishoot video ya wimbo wake ‘Kakopi Kapesti’ jijini Nairobi, Kenya.

Meninah amesema video ya wimbo wake huo imefanywa na Isaac, aliyeongoza video ya Prezzo ya wimbo wake ‘My Gal’. Amesema katika scene ambayo walikuwa wakihitaji moto, muongozaji aliandaa mapipa ya moto huku wakichukua tahadhari ya kuwa na fire extingusher kama lolote lingeweza kutokea.

Wakati wakishoot, walisikia mlipuko mkubwa wa moto uliosababishwa na mafuta yaliyokuwa yamewekwa pembeni ya mapipa ya moto.

“Hatua kama thelathini kulikuwa na gari limeegeshwa, yale mapipa mawili yote yakaruka kutokana na ule mlipuko, ile gari ya watu ikaangukiwa na yale mapipa,” alisema Meninah. “Tulichanganyikiwa, japokuwa tulikuwa na kibali lakini ni tatizo tayari limetokea. Lile gari tunaliona linateketea, mimi nilikuwa nalia, sikutegemea kwasababu ni gari la watu.”

Amesema polisi walikuja kwenye eneo hilo na kuwaweka chini ya ulinzi. “Tuliambiwa ‘wote mikono juu’, pigeni magoti’. Tulienda chini huku roho zetu zikiwa na huzuni na uoga,” alisema Meninah.

Tukio amesema lilivutia umati mkubwa wa watu waliokuja kuangalia kilichotokea kwakuwa moshi mzito ulikuwa umetanda angani. Walikaa chini ya ulinzi wa polisi hao kwa zaidi ya saa sita huku meneja akijaribu kuongea nao bila mafanikio. Polisi hao walichukua baadhi ya vitu vyao muhimu kama vitambulisho kikiwemo chake.

Polisi hao waliwapeleka kituo cha jirani na muda huo ikiwa ni saa 12 alfajiri. Hatua iliyofuata ilikuwa ni kupiga simu kwa wazazi wake Tanzania kuwaeleza hali halisi na kuomba msaada. Meninah amesema pamoja na baba yake kuwa nje ya nchi, alifanikisha kuwatumia fedha ambazo walichanga na muongozaji ili wamlipe mmiliki wa gari lililoungua.

“Mungu ni mkubwa sana, alitusimamia, ile hela ikaingia, mmoja wetu akatoka na afande akaenda kuchukua na yule mwenye gari akapewa pesa yake nusu kwasababu director hakuwa na pesa muda huo.”

Hata hivyo Meninah amesema video ya wimbo huo imekamilika na inaweza kutoka siku yoyote.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents