Habari

Gwajima ashindwa kufika mahakamani: Hukumu ya kesi yake yapigwa kalenda

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesogeza hukumu ya kesi inayomkabili Askofu wa Kanisa la ufufuo na uzima, Josephat Gwajima na wenzake watatu ya kushindwa kuhifadhi silaha na risasi hadi Agosti 30, 2017.

Askofu wa Kanisa la Ufufu na Uzima, Josephat Gwajima

Hukumu hiyo ilipaswa kutolewa leo Alhamisi, Julai 31 kwa Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha lakini ilishindikana kwa sababu hakimu huyo alikuwa na udhuru.

Wakili wa Askofu Gwajima, Peter Kibatala amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa wakati kesi ilipoitwa mbele yake kuwa Askofu Gwajima pia naye ni mgonjwa na mahakamani hapo amewakilishwa na mdhamini wake.

Hayo yametokea baada wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro kuiambia mahakama kuwa washtakiwa George Mzava, Msaidizi wa Askofu Gwajima, Yekonia Bihagaze (39) na George Milulu wapo mahakamani lakini Askofu Gwajima hayupo.

Pia, amedai kesi ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa hukumu lakini wamepata taarifa Hakimu Mfawidhi, Mkeha anayeisikiliza kesi hiyo anaudhuru.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo kesi imeahirishwa hadi Agosti 30, 2017 ambapo watasomewa hukumu.

Mzava, Bihagaze na Milulu wao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa wakimiliki bastola aina ya berretta pamoja na risasi 20 kinyume cha sheria.

Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa siku hiyo na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha mara baada ya mashahidi wa upande wa mashtaka na utetezi kutoa ushahidi wao na kuufunga.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali, Shedrack Kimaro na Joseph Maugo.

Huku upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Peter Kibatala ambapo washtakiwa walijitetea pamoja na mashahidi wao wawili akiwamo Nesi wa hospitali ya TMJ, Devotha Bayona .

By Godfrey Mgallah

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents