Siasa

Hatma ya Mbowe kujulikana leo

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi nchini Tanzania leo inatarajiwa kuamua iwapo Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini humo, CHADEMA, Freeman Mbowe ana kesi ya kujibu ama la katika tuhuma za ugaidi zinazowakabili.

Mbowe na wenzake watatu ambao walikuwa wanajeshi wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), Mohamed Ling’wenya, Halfan Bwire, Adam Kasekwa wanakabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwemo za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi.

Kitakachotokea kwenye uamuzi wa Mahakama hiyo leo ni kutamka kwamba Mbowe na wenzie iwapo wana kesi ya kujibu na hivyo kufungua milango kwa watuhumiwa hao kuanza kujitetea au kuifutilia mbali kesi hiyo na watuhumiwa hao kuachiwa huru.

Upande wa Jamhuri ulikamilisha kuwasilisha ushahidi wake wiki hii kupitia mashahidi wake 13 kati ya 24 waliotarajiwa kutoa ushahidi Mahakamani. Sehemu kubwa ya mashahidi hao 13 ni maafisa kutoka Jeshi la Polisi.

Tangu kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo namba 16/2021, kwenye Mahakama kuu divisheni ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, makundi ya wafuasi wa chama chake wamekuwa wakifika ndani na nje ya mahakama kufuatilia, huku ulinzi mkubwa ukiimarishwa wakati wote.

Mbowe alikamatwa pamoja na wafuasi wengine wa Chadema jijini Mwanza usiku wa kuamkia Julai 21, 2021 siku ambayo kulikua kufanyike kongamano kubwa la kudai katiba mpya lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha).

Siku chache kabla ya kukamatwa kwake, Polisi jijini Mwanza ilitangaza kuzuia kufanyika kwa kongamano hilo kwa sababu za kiusalama, lakini Mbowe alijitokeza mbele ya waandishi wa habari na kutangaza kwamba kongamano hilo lipo pale pale na litafanyika kama ilivyopangwa licha ya zuio hilo la Polisi.

“Kama polisi wanataka kutuzuia wajiandae kufanya hivyo wakiwa tayari kutukamata viongozi na wanachama wote kwa sababu sote hatutaondoka Mwanza hadi tufanye kongamano la Katiba mpya,” alisisitiza Mbowe katika mkutano huo na wanahabari.

Wafuasi wengine zaidi ya 10 waliokamatwa pamoja na Mbowe jijini Mwanza waliachiliwa huru na jeshi la polisi, ambapo Mbowe aliendelea kushikiliwa kabla ya kuunganishwa na wanaodaiwa kuwa walinzi wake kwenye kesi inayoendelea sasa ya ugaidi.

Katika kesi hiyo Mbowe anadaiwa kula njama ya kutenda kosa la ugaidi kati ya Mei na Agosti mwaka 2020 akiwa katika Hoteli ya Aishi Mkoani Kilimanjaro, kosa la pili la Mbowe ni kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi kinyume cha sheria ya ugaidi kati ya tarehe hizo tajwa.

Haya ni matukio muhimu ya kesi hii inayofuatiliwa kwa ukaribu ndani na nje ya nchi:

Julai 21, 2021: Mbowe alikamatwa

Kiongozi huyu mkuu wa Chadema alitiwa mbaroni huko jijini Mwanza usiku wa kuamkia tarehe 21 mwezi Julai, 2021. Chama chake cha Chadema, kiliwataka wafuasi wa chama hicho kuingia mtaani kumtafuta baada ya juhudi zake za kumtafuta kukwama na hawajui walipo, baada ya Mamlaka kutosema lolote kwa muda kuhusu kukamatwa kwa Mbowe. Baadae Polisi walikuja kuthibitisha kumkamatwa na kwamba amesafirshwa kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam na kuunganishwa kwenye kesi ya ugaidi.

Taarifa ya Msemaji wa Polisi, David Misime ilisema kuwa Mbowe hakukamatwa kwa tuhuma za kupanga na kuandaa kongamano la Katiba mpya jijini Mwanza bali alifahamu tuhuma zinazomkabili.

Julai 26, 2021: Kufikishwa mahakamani

Mbowe alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza Julai 26, 2021 na kusomewa mashtaka mawili ikiwemo la ugaidi. Baada ya kusomewa maelezo Mbowe hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka, kesi ikahairishwa hadi Agosti 5, 2021 kusubiri nyaraka ili ihamishiwe Mahakama kuu.

Agosti 6, 2021 Asomewa Mashitaka

Mbowe ambaye ni kiongozi wa zamani wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB) na wenzake watatu walisomewa mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa kufanya vitendo hivyo.

Mashtaka mengine ni kukusanya fedha kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi, kukutwa na silaha aina ya bastola na kukutwa na sare za jeshi kinyume cha sheria. Kati ya mashtaka hayo sita, Mbowe anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi.

Agosti 9, 2021: Rais Samia azungumzia Kesi ya Mbowe

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan licha ya kusema hawezi kuzungumzia zaidi kesi ya Mbowe kwa kuwa iko Mahakamani, aliiambia BBC kuwa mashtaka dhidi ya kiongozi huyo wa Upinzani hayakuchochewa kwa sababu za kisiasa.

Pamoja na mengine kauli yake hiyo iliibua mjadala mzito kwa wafuatiliaji wa kesi hiyo na siasa za Tanzania kwa ujumla.

Septemba 03, 2021: Kuanza kusikilizwa kwa kesi

Kesi hii ilianza kusikilizwa kwenye Mahakama kuu ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ikitokea Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu ambayo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kisheria.

Septemba 6, 2021: Jaji Luvanda ajitoa kusikiliza kesi

Jaji Elinaza Luvanda alijitoa kusikiliza kesi hiyo kufuatia maombi ya Mbowi, kwa niaba ya washitakiwa wenzake kudai kuwa hawana Imani na Jaji huyo kama atatenda haki. Nafasi yake akapangiwa Jaji Mustapha Siyani.

Oktoba 20, 2021 Jaji Siyani ajitoa kusikiliza kesi

Jaji Mustapha Siyani alikuwa jaji wa pili kujitoa kusikiliza kesi hiyo kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Jaji kiongozi. Jaji Joachim Tiganga akachukua nafasi yake

Februari 13, 2022: Ushahidi kufungwa

Ushahidi umefungwa Wiki hii Februari 13, 2021 kwa mashahidi 13 wa upande wa mashtaka kumaliza kutoa ushahidi wao. Kinachosubiriwa sasa ni uamuzi wa Mahakama Kuu hiyo kuamua leo kama Mbowe na wenzie wana kesi ya kujibu ama la.

Chanzo BBC.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents