Siasa

Haya ndio mambo waliyozungumza Rais Samia Suluhu na Tundu Lissu

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Jumatano Februari 16, 2022 amefanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu Mjini Brussels nchini Ubelgiji.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano wa rais, Ikulu ilitumwa kwenye mitandao ya kijamii pamoja na picha mbalimbali za mkutano huo.

Baadaye kupitia mtandao wake wa Twitter, Tundu Lissu alieleza mambo makuu sita yaliyotawala katika mazungumzo hayo.

1. Kesi ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe

Jambo la kwanza ni kuhusu kesi ya mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Lissu anasema jambo la kwanza alilozungumza na rais Samia ni kuondolewa kwa kesi ya Mbowe.

Mbowe anakabiliwa na mashtaka kadhaa ikiwemo ugaidi na kesi yake inaendelea mahakamani nchini Tanzania.

Mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Tanzania

2.Haki za vyama vya upinzani

Kuhusu haki za vyama vya siasa hususani vyama vya upinzani.Amesema amemueleza Rais Samia katika mkutano wao, aangazie suala la haki za kisheria za vyama vya upinzani ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa. Lissu amebainisha kuwa wamezungumzia suala hilo kwa kina na kuwa rais Samia ameahidi kulishughulikia.

3. Katiba Mpya

Kuhusu Katiba Mpya, Lissu amesema jambo jingine ambalo amezungumza na Rais Samia ni kuhusu kuanzisha mchakato wa katiba mpya.Anasema kuwa Rais Samia ana nafasi kubwa ya kuachia nchi ya Tanzania katiba mpya na ya kidemokrasia. ”Tumezungumza kwa kirefu, nimemwambia rais mjadala wa katiba mpya utakuwa mrefu, lakini ni muhimu kama taifa tujadili suala hili muhimu”

4. Maslahi ya Tundu Lissu

katika ajenda hii Lissu amesema ni wakati sasa wa kupatiwa haki zake zote, ikiwemo kupatiwa matibabu na mazingira yote ya kuondolewa kwake bungeni kinyume na sheria na pia kulipwa kiinua mgongo chake kama sheria za Tanzania zinavyosema.

Hatahivyo, akizungumza mwaka juzi aliyekuwa spika wa bunge la Tanzania, Job Ndugai alisema Lissu alipokea takriban shilingi milioni 500 za kitanzania kufikia mwezi Juni 2019 zikiwemo shilingi milioni 200 za mishahara yake na shilingi milioni 360 za posho akiwa Ubelgiji, jambo ambalo Lissu amekanusha.

5.Suala la Lissu kurejea nyumbani

Ameongeza pia suala lingine ni kuhusu kurejea kwake nyumbani Tanzania, amesema kuwa Rais Samia ahakikishe atakuwa salama pale atakaporudi, yeye pamoja na wenzake waliopo uhamishoni, akiwemo Godless Lema na Ezekiel Wenje, wote wanachama wa Chadema.

6. Wabunge viti Maalum Chadema

Tundu Lissu amesema wabunge hao akiwemo Halima Mdee, Esther Bulaya na wenzake hawana uhalali wa kukaa bungeni kwasababu chama chao kiliwafukuza. ”Haijalishi suala la rufaa, suala la rufaa ni tofauti kabisa, kwa sasa si wanachama wa Chadema, nimemwambia mheshimiwa rais alishughulikie hilo” anasema Lissu.

Tundu Lissu: Rais amenipokea vizuri, amenisikiliza na mimi nimemueleza yote niliyotaka kumueleza

Ajenda ya mwisho katika mkutano huo, amesema ilikuwa ajenda ya ujumla ambayo ni Rais Samia kuongoza nchi ya Tanzania akiwa na jukumu la kipekee kuongoza na kusaidia kuponya nchi ya Tanzania. ”Watu wengi wameumizwa katika kipindi hiki cha miaka sita tangu mwaka 2015, nimemwambia, mheshimiwa rais kuwa yeye ndiye ambaye ana jukumu na fursa ya kuponya marejaha haya, kuponya vilio hivi”

Lissu amemalizia kwa kusema kuwa nafasi ya mazungumzo baina yake na rais Samia ni jambo la muhimu sana, na amemshukuru Samia kwa kumpatia fursa hiyo ya mazungumzo.

Tundu Lissu

Amewataka pia wafuasi wake kuungana naye na kushirikiana na Samia ili kujenga nchi mpya yenye maendeleo.

Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi Septemba 2017 mjini Dodoma akitoka katika shughuli zake bungeni.

Baada ya shambulio hilo Lissu alisafirishwa kwa ndege hadi Hospitali ya Nairobi, Kenya ambako alitibiwa kabla ya kuhamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu maalumu.

Alirejea Tanzania na kushiriki uchaguzi mkuu akigombea urais kupitia Chadema. Siku chache baadaye aliondoka Tanzania na kurudi Ubelgiji skisema ni kwa sababu za kiusalama.

Mkutano huo baina ya Samia na Lissu umeleta hisia mbalimbali kwa wanasiasa na wanaharakati nchini Tanzania wengi wakidai kuwa ni dalili nzuri ya kidemokrasia na siasa za maridhiano.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents