Habari

Hii ndio sababu iliyoifanaya Marekani kuanza kuondoa wanajeshi wake Syria

Baada ya siku kadhaa za mvutano juu ya tamko la rais wa Marekani Donald Trump kwamba ataondoa majeshi yake nchini Syria, afisa mmoja wa kijeshi amesema hatua hiyo imeanza kutekelezwa huku akikataa kuizungumzia zaidi. Kanali Sean Ryan, msemaji wa muungano wa kijeshi  unaoongozwa na Marekani unaopambana na wanamgambo wa dola la kiislamu amesema mipango ya kuondoka kwa maksudi nchini Syria imeanza.

“Kufuatia wasiwasi juu ya usalama wa operesheni hii hatutajadili lolote juu ya maeneo au mienendo ya wanajeshi hawa,” alisema Sean Ryan. Bado hapajakuwa na taarifa zaidi kuhusu kuondoka kwa wanajeshi hao, magari mangapi yalioondoka au hata iwapo kuna wanajeshi kadhaa ambao tayari wameshaondoka nchini humo.

Kwa mujibu wa dw, Shirika la Uingereza la uangalizi wa haki za binaadamu lililo na makao yake nchini Syria na linalofuatilia hali ya kivita nchini humo limesema Marekani ilianza kuwaondoa wanajeshi wake tangu jana usiku. Shirika hilo, limesema msafara wa magari takriban kumi ulionekana ukiondoka kutoka Kaskazini Mashariki mwa mji wa Rmeilam na kuelekea nchini Iraq.

Kuthibitishwa huku kwa wanajeshi wa Marekani kuanza kufunga virago kumekuja baada ya kuwepo kwa taarifa za kukanganya kuhusu mipango ya kutekeleza amri ya Trump ya majeshi yake kuondoka nchini humo na vitisho kutoka Uturuki kuwashambulia wakurdi washirika wa Marekani  katika vita vya nchi kavu  dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislamu IS.

Kuna takriban wanajeshi  2000 wa Marekani nchini Syria. Hatua ya kushtukiza ya Trump mwezi Desemba ya kuwaondoa wanajeshi hao, akisema tayari wamelishinda nguvu kundi la wanamgambo la IS iliwashitua wengi na kukosolewa na baadhi ya majenerali wake pamoja na washauri wa usalama wa kitaifa na kusababisha mkwamo wa serikali ya Marekani.

Huku hayo yakiarifiwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, alioko ziarani Mashariki ya Kati amewahakikishia wakurdi usalama wao baada ya vikosi vya Marekani kuondoka nchini humo. Hata hivyo maafisa wa kikurdi wametaka ufafanuzi juu ya nia ya Marekani kuondoka na kuwaacha katika hatari ya kushambuliwa na Uturuki  kwa upande mmoja na vikosi vya rais Bashar al Asaad kwa upande mwengine.

Wakati huo huo msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova amesema wamarekani hawana uhakika wa kuondoka Syria. Akizungumza na waandishi habari mjini Moscow amesema wanadhani bado Marekani inafikiria sababu ya kuendelea kuwepo Syria.

Ameongeza kuwa hawajaona taarifa ya wazi inayoelezea mkakati wa Marekani nchini Syria na hawawezi kuwa na uhakika juu ya Marekani kuondoka nchini humo.

Vikosi hivyo vimekuwa Syria tangu mwaka 2014 wakati kundi la kwanza liliwasili kutoa ushauri kwa wanapiganaji wa kikurdi waliokuwa wanapambana na dola la kiislamu.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents