Habari

Historia, Rais Dkt. Samia akizindua ujazaji maji Bwawa la Nyerere

Leo Desemba 22, 2022 Tanzania inaandika historia katika safari kuelekea mapinduzi ya nishati ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua zoezi la kuanza kujaza maji katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 78.68.

Katika hafla hiyo itakayofanyika eneo la mradi na kuhudhuriwa na takribani watu 3,000, Dkt. Samia atabonyeza kitufe ambacho kitafunga handaki la kuchepusha maji, hivyo kuruhusu maji kuanza kuingia kwenye bwawa hilo la ujazo wa lita bilioni 32.

Hatua hiyo ni kubwa katika utekelezaji wa mradi huo ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 2,115 ambazo zitatosheleza mahitaji ya sasa nchi nzima, na kuwa kichocheo cha kuvutia wawekezaji kutokana na kuwa na umeme wa uhakika unaotosheleza.

Mbali na hayo, bwawa hilo ambalo utekelezaji wake ulianza wakati wa uongozi wa Hayati Mwl. Julius Nyerere litachochea ukuaji wa sekta nyingine kama kilimo, kwa kuwezesha kilimo cha umwagiliaji, utalii, kutokana na kuwa katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, litamaliza changamoto ya mafuriko na pia kukuza uvuvi, ambapo litakuwa ziwa kubwa, likiyazidi baadhi ya maziwa ya asili nchini.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Maharage Chande, ujazaji maji unatarajiwa kukamilika mwaka 2024, na uzalishaji wa umeme utaanza Juni mwaka huo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents