Habari

Hotuba ya Mh. Zitto mkoani Tabora

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe katika hotuba yake ya uchaguzi mdogo kwenye kata ya Muungano,Urambo nzima na Tabora kwa ujumla amezungumzia masuala machache ya kitaifa ambayo kwa kiasi kikubwa ameeleza kuwa yanawagusa watu wa maeneo hayo.

Hotuba aliyoitoa katika maeneo hayo ni hii ifuatayo:

Serikali Inunue Tumbaku yote Kuwaokoa Wakulima.

Sehemu ya Hotuba ya Kiongozi wa Chama katika Mkutano wa Kampeni, Kijiji cha Kalemela A, Kata ya Muungano, Urambo, Mkoani Tabora. Novemba 16, 2017

Ndugu wananchi wa Kalemela,
Pamoja na masuala haya ya uchaguzi mdogo hapa kwenye kata yenu ya Muungano, ninaomba nizungumzie masuala machache ya kitaifa ambayo kwa kiasi kikubwa yanawagusa nyie watu wa Muungano, Urambo nzima na Tabora kwa ujumla.

Shughuli kuu yenu ya uchumi ni Kilimo, lakini tangu Mwaka 2015 ukuaji wa sekta ya Kilimo umekuwa ukushuka. Mwaka 2016 Sekta ya Kilimo imekua kwa wastani wa asilimia 2.1 tu, na ukilinganisha na ukuaji wa idadi ya watu ya asilimia 2.8 maana yake ni kwamba Watanzania wengi wanashindwa hata kupata chakula. Tunazalisha watu zaidi kuliko chakula, ni dhahiri tunaelekea kubaya. Miaka miwili ya Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano mmekuwa masikini zaidi.

Nchini kwetu zaidi ya 65% ya wananchi wote wanashughulisha na Kilimo, kwa vijijini ni zaidi ya 78%, hapa kwenu 90% yenu ni wakulima. Kilimo pia ndio tegemeo la uhakika wa chakula kwa 100%. Wakati ukuaji wa kilimo unashuka kila mwaka, bajeti ya Serikali ya Maendeleo ya Kilimo kwa mwaka 2016/17 ilitekelezwa kwa 3% (ikipangwa shilingi bilioni 101 na ikitumika shilingi bilioni 3.7 tu), hivyo kuondoa hata uhakika wa kupata chakula.

Katika hali hiyo ya kudumaa kwa kilimo chetu kwa ujumla nchini, nyie wakulima wa Tabora bado mmetufuta machozi, zao lenu la Tumbaku ndio zao la kwanza kwa kuliingizia Taifa letu fedha za kigeni, mkiwa mbele ya Korosho iliyoliingizia Taifa Dola milioni 300.47 kwa mwaka 2016, japo kwa mwaka huu wa 2017 korosho imekuwa ya kwanza.

Mwaka huo wa 2016, thamani ya mauzo ya tumbaku iliongezeka kwa 8.7% na kufikia wastani wa dola za Marekani milioni 312.7, ikilinganishwa na dola milioni 287.6 mwaka 2015. Ongezeko hili la thamani lilitokana na kuongezeka kwa wastani wa bei ya tumbaku katika soko la dunia kutoka dola 4,336.5 kwa tani mwaka 2015 hadi wastani wa dola 4,732.0 kwa tani mwaka 2016.

Kwa upande mwingine, kiasi cha tumbaku iliyouzwa nje ilipungua hadi tani 66,091 mwaka 2016 kutoka tani 66,326 mwaka 2015. Tunajua kuwa duniani kote kuna juhudi za kupiga vita uvutaji wa sigara na hivyo mahitaji (demand) ya Tumbaku duniani yanashuka. Vile vile kuna suala la uharibifu wa mazingira kama vile kukata miti kwaajili ya kukaushia tumbaku nk, na hivyo kufanya Tumbaku kuwa zao linalopaswa kuachwa na kubadilishwa.

Ninatambua juhudi za kuanza kulima Mikorosho kama zao mbadala. Juhudi ambazo naziunga mkono kwa dhati. Kuna maeneo ya Tabora ambayo yanaweza kulima Michikichi ambayo ina faida kubwa na ni zao la kuondoa umasikini. Sisi Kigoma tutakuwa tayari kushirikiana nanyi katika mabadiliko hayo. Hata hivyo, wakati michakato hiyo inafanyika ni lazima tuwe na jawabu la Tumbaku yenu ambayo haijapata soko.

Nimezunguka leo vijiji vyote 4 vya kata hii ya Muungano na kila mahala naona nyuso za huzuni kubwa kutoka Kwa wananchi. Nikiuliza naambiwa Tumbaku ya mwaka Jana haijauzwa na msimu mpya umeanza. Maana yake ni kwamba wakulima mmeingia msimu mpya ilhali mavuno ya msimu uliopita hayajauzwa. Hamjalipa mikopo ya pembejeo, hamjapata pesa ya kulipia huduma za muhimu za familia zenu, na nimeambiwa kuwa hata kula sasa ni mlo mmoja kwa siku. Inasikitisha sana.

Nimefuatilia suala hili na kugundua kuwa wanunuzi wa Tumbaku walinunua kiasi walichoingia mikataba na vyama vyenu vya Msingi na mavuno yote ya ziada yamekosa soko. Kwa Tabora peke yake, Tumbaku ya zaidi ya Tani 13,000 (zaidi ya 20% ya mauzo nje ya mwaka 2016), yenye thamani ya dola za kimarekani 62 milioni (shilingi bilioni 150), inaoza kwenye maghala ya vyama vya Msingi. Urambo peke yake ina zaidi ya nusu ya tani hizo. Nawapa pole sana kwa kadhia hii. Hizi ni pesa nyingi sana kuingia kwenye uchumi wa Tabora Lakini hakuna hatua Serikali imechukua.

Wananchi wa Kalemela, Serikali hii ilipoingia madarakani ilihimiza watu kufanya kazi. Mmefanya kazi na kuzalisha ziada. Serikali hii inasema mmezalisha kingi mno. Mnaadhibiwa kwa kufanya kazi na kuzalisha ziada. Huu ni mzaha. Hii ni Serikali inayowaza Bombadier na mabarabara ya juu (mafly over) ya Dar es salaam, na sio ninyi wanyonge wakulima wa hapa kijijini Kalemela, wakulima wa Urambo na Tabora. Ikataeni Serikali hii kwa kura kwenye uchaguzi huu wa diwani wa kata yenu. Muitie adabu kwa kutowajali.

Serikali makini ingefanya nini kwenye kadhia hii ya Tumbaku? Sisi ACT Wazalendo tungekuwa madarakani tungenunua Tumbaku yote ya ziada ya wakulima kwa kutumia kasma ya fedha za dharura kwenye Fungu la 50 Wizara ya Fedha. Kisha Serikali ingetafuta soko kwa mfumo unaoitwa G to G yaani Government to Government na kuuza Tumbaku hiyo na kurejesha fedha hizo kwenye mfuko wa dharura.

Ninaamini kuwa Serikali hii ya CCM ya awamu ya tano ina uwezo huo Lakini haina dhamira na MAARIFA ya kuwasaidia wananchi wake. Serikali hii ipo tayari kutumia shilingi trilioni moja kulipia ndege ambazo ni Watanzania 5% wanapanda kuliko kuokoa wakulima milioni 1.4 wa Tumbaku nchi nzima kwa shilingi bilioni 150 tu, tena ikiwa fedha hizo zinarudi ndani ya muda mfupi.

Wananchi wa Kijiji cha Kalemela, tarehe 26 Novemba twende kumchagua mgombea udiwani wa ACT Wazalendo ili tupaze sauti tumbaku yenu ya mwaka jana inunuliwe. Tuishinikize Serikali inunue tumbaku yote na kuondoa adha hii kwenu. Serikali itafute masoko Tumbaku ikiwa yao na sio yenu. Serikali hii ya CCM haitasikia kama hamtainyima kura.

Wananchi wa Urambo, niwakumbushe kuwa Ilani ya Uchaguzi ya chama cha ACT Wazalendo ilitangazwa na Taasisi ya MVIWATA kuwa ilani bora zaidi kuhusu masuala ya Kilimo kuliko ilani za vyama vyote katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Katika ilani ile tulipendekeza kuwapo kwa Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima.

Mfumo wa Akiba ya Hifadhi ya Jamii ungekuwa jawabu tosha kwenye kadhia ya Tumbaku mnayopata sasa kwani Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ungewalipa fedha za tumbaku na wao wangeweza kutafuta wateja na kuiuza kwa kupitia Fao la Bei. Serikali ya CCM haina wala haiwazi MAARIFA ya namna hiyo. Nawasihi msiwachague. Naomba kura kwa ndugu Kazimoto wa ACT Wazalendo awe diwani wenu kwenye kata ya Muungano.

Nawashukuru sana kwa kunipokea kwa wingi na kuhudhuria mkutano wetu huu mkubwa hapa Kijijini, Kalemela Wilayani Urambo.

Ahsanteni sana.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Kijiji cha Kalemela – Kata ya Muungano
Urambo
Tabora

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents