Habari
Kenya: Vigogo 27 watumbuliwa sababu ya sukari
Kenya imewasimamisha kazi zaidi ya maafisa 20 baada ya tani 1,000 ya sukari iliyogunduliwa kuwa si salama kuuzwa madukani nchini humo.
Kwenye taarifa, Felix Koskei, mkuu wa watumishi wa umma katika serikali ya Rais William Ruto, alisema jana Jumatano kwamba sukari hiyo iliyoagizwa mwaka 2018 ilishaharibika kwa kuwa muda wake wa matumizi ulishapita.
Licha ya kutangazwa kuwa si salama kwa matumizi, sukari hiyo iliruhusiwa masokoni, hatua ambayo Koskei amesema ni kinyume na utaratibu na kitendo cha kihalifu.
Koskei amesema maafisa 27 wamesimamishwa kazi akiwemo mkuu wa halmashauri inayosimamia viwango vya ubora wa bidhaa, maafisa wa polisi na maafisa wa mamlaka ya kodi na vyakula nchini humo.