Habari

Kim Jong Un aitupia lawama Marekani kuzorotesha usalama wa rasi ya Korea

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ameitupia lawama Marekani akiitaja kuwa chanzo cha wasiwasi katika rasi ya Korea, huku akiutetea mpango wa taifa hilo wa kujiimarisha kijeshi.

Nordkoreas Machthaber Kim Jong Un

Kim Jong Un, ameutetea mpango wake wa kujiimarisha kijeshi akisema ni mkakati wa kujilinda dhidi ya sera za uchokozi za Marekani lakini pia hatua za kujiimarisha kijeshi za Korea Kusini zinazozidisha wasiwasi kwenye rasi hiyo.

Mapema leo, Kim Jong Un amesema wakati wa hotuba ya ufunguzi wa maonyesho ya kijeshi kwamba Marekani ndio hasa chanzo cha mzozo na wasiwasi kwenye rasi ya Korea. Taarifa hii ni kulingana shirika rasmi la habari la Korea.

Kim amenukuliwa akisema hakukuwa na msingi wowote wa Marekani kuchukua hatua dhidi yake, na kwa upande mwingine ikisema haina mvutano wowote na taifa hilo. Serikali ya rais Joe Biden mara kadhaa imesema haina nia yoyote ya uchokozi dhidi ya Korea Kaskazini, lakini Kim ameliambia kusanyiko kwenye maonyesho hayo kwamba ana wasiwasi iwapo kuna mtu ama taifa lolote litaamini matamshi hayo.

Kim anatoa matamshi hayo baada ya taifa hilo kufanya majaribio ya makombora ya masafa marefu wiki kadhaa zilizopita na kusisitiza kwamba lengo la taifa lake ni kujiimarisha kijeshi na kufikia kiwango cha juu kabisa kiasi kwamba hakutakuwa na yoyote atakayejaribu kupambana na Korea Kaskazin

Kim aikosoa Korea Kusini kwa undumila kuwili.

Pamoja na kuituhumu Marekani kwa kuvuruga ustahmilivu kwenye rasi ya Korea, Kim ameikosoa vikali Korea Kusini akiita ndumila kuwili kutokana na kupinga hatua zake za kujiimarisha kisilaha ambazo Korea Kusini inasema ni za uchokozi. Hata hivyo Korea Kusini nayo imekuwa ikitumia fedha nyingi kujiimarisha kijeshi, ikiwa ni pamoja na kununua ndege za kisasa zaidi za kivita kutoka Marekani.

Lakini kwa mara nyingine, Kim amesema hawana malengo ya kupambana na jirani yake Korea Kusini na kuongeza kuwa hawataki kurudia historia mbaya ya kutumia nguvu baina yao, ingawa luteka za pamoja za kijeshi za Korea Kusini na Marekani zimekuwa zikiigadhabisha Korea Kaskazini, ambayo inahisi ni maandalizi ya kuivamia.

Washington na Seoul ni washirika wa kiusalama, na Washington ina takriban wanajeshi 28,500 Korea Kusini wakisaidia kumlinda dhidi ya jirani yake, aliyewahi kumvamia mnamo mwaka 1950.

Pyongyang inakabiliwa na vikwazo kadhaa vya kimataifa kutokana na mipango yake ya nyuklia na makombora iliyoongezeka kwa haraka chini ya uongozi wa Kim. Mwaka 2017, ilifanya majaribio ya makombora yanayoweza kufika bara zima la Marekani na imeendelea kusisitiza kwamba inahitaji silaha madhubuti za kujilinda na uvamizi wa Marekani.

Mwaka 2018, Kim alikuwa kiongozi wa kwanza wa Korea Kaskazini kukutana na rais wa Marekani Donald Trump katika mkutano wa kilele nchini Singapore. Lakini hata hivyo mazungumzo yamezorota, tangu walipokutana kwa mara ya pili mjini Hanoi. Serikali ya Biden inasema iko tayari kukutana na maafisa wa Korea Kaskazini wakati wowote na bila ya masharti katika juhudi za kupunguza shughuli hizo za nyuklia za Korea Kaskazini.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents