Habari

Mambo 10 yakuyafahamu kuhusu bajeti ya Wizara ya Nishati

Waziri wa Nishati, January Makamba @jmakamba jana amewasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2022/2023 ambapo katika bajeti hiyo amezungumzia mambo mbalimbali, haya ni mambo kumi ambayo pia ni muhimu kuyafahamu.

1. UJENZI WA VITUO VIDOGO VYA KUSAMBAZA BIDHAA ZA PETROLI VIJIJINI.
Watanzania wengi vijijini wanalipa fedha nyingi zaidi kununua nishati ya mafuta, ambayo pia sio safi na salama. Kutibu kadhia hiyo, serikali imebuni mradi wa uwezeshaji na uendelezaji wa vituo vidogo vya bidhaa za petroli kwa maeneo ya vijijini ambayo hayana vituo vya mafuta kwa njia ya mkopo nafuu. Mradi huu ni mpya na kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kuandaa wigo wa mradi, kutangaza zabuni na kuwapata waendelezaji wadogo wadogo wa vituo vya mafuta vijijini ili kuanza ujenzi wa vituo hivyo.
#DiraMpyaNishati

2. UANZISHWAJI WA UKANDA MAALUM WA UCHUMI KATIKA ENEO LA MRADI WA LNG – LINDI.
Serikali ina mpango wa kuanzisha Ukanda Maalum wa Kiuchumi (Special Economic Zone) katika eneo la mradi wa LNG – Lindi, ambapo maeneo yatatengwa na kuendelezwa kwa ajili ya uwekezaji, uzalishaji na biashara. Hatua hii, pamoja na kuimarisha shughuli za kiuchumi wakati wa utekelezaji wa mradi, pia itawezesha manufaa ya mradi kuendelea kupatikana hata baada ya ukomo wake.
#DiraMpyaNishati
3. HIFADHI YA KIMKAKATI YA MAFUTA UAGIZAJI, UHIFADHI NA USAMBAZAJI.
Uanzishwaji wa Hifadhi ya Kimkakati ya Mafuta (Strategic Petroleum Reserve – SPR) unahusisha uratibu wa uagizaji, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za mafuta kwa kipindi mahsusi. Uanzishwaji wa SPR ni muhimu ili kuwezesha usalama na uhakika wa usambazaji mafuta nchini wakati wote. Ushiriki wa Serikali katika kuwezesha kuwepo kwa SPR utawezesha nchi kuwa na akiba ya mafuta muda wote na kuwezesha shughuli za uchumi kutoathiriwa na matukio yanayovuruga mwenendo wa bei za mafuta.
#DiraMpyaNishati

4. KIGOMA NA KATAVI KUUNGANISHWA NA GRIDI YA TAIFA.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, sio tu kwamba umeme wa Gridi ya Taifa utafika Kigoma, bali pia umeme unaoingia kwenye Gridi ya Taifa utazalishwa Kigoma Kutumia Maji wa Malagarasi.
#DiraMpyaNishati
5. UMEME JUA, UPEPO NA MAPOROMOKO YA MAJI IMEPATA WAWEKEZAJI.
Wizara kwa kushirikiana na TANESCO imeandaa miradi 53 ya umeme yenye sura ya kutekelezwa kupitia Sekta Binafsi. Hadi sasa, miradi saba (7) ya umeme jua, upepo na maporomoko ya maji yenye uwezo wa kuzalisha MW 597 ilipata wawekezaji wenye nia ya kuiendeleza.
#DiraMpyaNishati
6. VITUO VYA KUJAZIA GESI ASILIA KWENYE MAGARI.
Serikali kupitia TPDC imepanga kutekeleza mradi wa ujenzi wa vituo vya kujazia Gesi asilia kwenye Magari katika Bohari Kuu za mafuta za Serikali za Dar es Salaam na Dodoma. Lengo ni kuwezesha magari mengi zaidi ya Serikali na watu binafsi kutumia gesi asilia inayozalishwa nchini badala ya Mafuta.
#DiraMpyaNishati
7. KUBADILISHA DENI LA TANESCO KUWA HISA.
Serikali pia inatafakari namna sahihi ya kutekeleza mpango wa kubadilisha deni la TANESCO kwa Serikali kuwa hisa za Serikali (Debt to Equity Conversion) ili kuweka vitabu vya mahesabu vya Shirika katika hali nzuri itakayoliwezesha Shirika kupata fedha za miradi bila kutegemea Serikali.
#DiraMpyaNishati
8. TANESCO NA TRC KUSHIRIKIANA UMEME WA UHAKIKA.
TANESCO kwa kushirikiana na Shirika la Reli Nchini (TRC) itaendelea kuhakikisha miundombinu ya umeme msongo wa kV 220 yenye urefu kwa kilomita 415 inakamilika kuhakikisha uhakika wa umeme kwenye reli ya SGR’ – @JMakamba
#DiraMpyaNishati

9. SERIKALI YATENGA VITALU VYA MAFUTA NA GESI KIMKAKATI.
Serikali ilitenga vitalu vya mafuta na gesi vya kimkakati kwa ajili ya kuipatia TPDC ili kuijengea uwezo na uzoefu. Vitalu hivyo ni Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi-Wembere, Songosongo Magharibi. Ziwa Tanganyika na 4/1B na 4/1C. Katika mwaka wa fedha wa 2022/23, Serikali imetenga kiasi kwa shilingi bilioni 102.167 kwa ajili ya kazi mbalimbali za maandalizi ya uchimbaji wa gesi na mafuta kwenye vitalu hivyo.
#DiraMpyaNishati
10. TANZANIA KUSAMBAZA GESI NCHI ZA KENYA NA UGANDA.
Serikali ina makubaliano ya awali (MoU) na nchi za Uganda na Kenya kwa ajili ya ujenzi wa mabomba ya kusafirishia gesi asilia kutoka Tanzania kwenda kwenye nchi hizo. Miradi yote ipo katika hatua za awali, ikiwemo matayarisho ya kufanya upembuzi yakinifu. Kwa upande wa mradi wa bomba la kwenda Uganda, Serikali imetenga shilingi milioni 635 na upande wa bomba la kwenda Kenya shilingi milioni 656.10 kwa ajili ya kazi mbalimbali za awali.
#DiraMpyaNishati

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents