Habari

Mashabiki, wanachama wa Yanga wajitokeza kuchangia damu

Na Janeth Jovin

Rais wa Klabu ya Soka ya Yanga Mhandisi Hersi Said amesema klabu hiyo katika kuelekea wiki ya wiki ya mwananchi imeamua kuwahamasisha mashabiki na wanachama wake kujitokeza kuchangia damu katika vituo vilivyoanishwa nchi nzima ikiwa ni sehemu ya mchango wa klabu hiyo kwa jamii.

Mhandisi Hersi amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa zoezi la uchangiaji damu liliondaliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na Klabu hiyo liliofanyika MNH-Mloganzila ambapo pia amewashauri mashabiki na wanachama wa Klabu ya Yanga kuendelea kujitokeza kwa wingi kuchangia damu kwa lengo la kuisaidia jamii.

“Tunayo furaha kushiriki katika matukio haya ya kijamii, mashabiki na wanachama wetu wameonesha uungwana mkubwa sana kwakuwa wamechangia damu bila hata kujua ni nani ataenda kuwekewa damu hiyo, nawapongeza sana na pia nawasihi Watanzania wengine kuiga moyo huu” amesema Mhandisi Hersi.

Mmoja wa wanachama wa Yanga (aliyevaa jezi) akichangia damu

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi ameipongeza klabu hiyo kwa uamuzi wa kuchangia damu ambapo amesema mahitaji ya damu kwa MNH-Mloganzila ni kati ya chupa 30 hadi 35 na Upanga chupa 100 hadi 150 kwa siku.

Prof. Janabi ameongeza kuwa mtu akitoa damu haimaanishi kwamba damu itaisha mwilini kwakuwa chembe chembe za damu huishi kati ya siku 90 hadi 120 ambapo hufa na kuzalishwa zingine hivyo jamii isiwe na hofu ya kuchangia damu.

Pia Prof. Janabi amebainisha kuwa baada ya kutolewa kutoka kwa mchangiaji zipo hatua mbalimbali zinafuatwa kabla kuwekwa kwa mgonjwa ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi wa usalama wa damu yenyewe ikiwa ni pamoja na kuangalia maambukizi ya virusi vya homa ya ini, VVU na maradhi mengine na kuongeza kuwa haya yote hufanywa kwa lengo la kujiridhisha kuwa damu anayowekewa mgonjwa ni salama.

Aidha, Prof. Janabi ameishauri jamii na vilabu vingine vya soka vinavyoshiriki ligi kuu kuiga mfano huu wa Klabu ya Yanga wa kuchangia damu kwa kuwa damu itakayotolewa itawasaidia mama wajawazito, wagonjwa wa saratani, wananchi wanaofanyiwa upasuaji na majeruhi wa ajali mbalimbali.

Waliochangia damu katika zoezi la leo wamepewa tiketi ya kushuhudia mchezo kati ya klabu hiyo na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini utakaofanyika tarehe 22.07.2023 katika uwanja wa Benjamin Mkapa maarufu Lupaso mkoani Dar es Salaam.

Hii ni mara ya pili kwa Klabu ya Yanga kushiriki katika zoezi hilo ambapo leo Injinia Hersi ameambatana na Kocha Mkuu wa klabu hiyo Bw. Miguel Gamondi, zaidi ya uniti 100 zitarajiwa kukusanywa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents