Habari

Msajili wa Hazina afichua ukweli hali mbaya za benki

Msajili wa Hazina nchini, Lawrence Mafuru amesema benki nchini zinashindwa kueleza ukweli juu ya kuyumba kwao na kwamba madai hali zao ni mbaya kutokana na agizo la serikali la kutaka fedha zake zitunzwe Benki Kuu ya Tanzania (BOT), hayana ukweli.

benki-mafuru_478_306

Akizungumza Jumatano hii jijini Dar es Salaam, Msajili huyo amesema licha ya kukiri kuwa mzunguko wa fedha umepungua kutokana na Tanzania kuchagua kwamba fedha inazozipata zitumike katika miradi ya maendeleo badala ya matumizi ya kawaida, benki zinazolalamika zimeshindwa kurejesha fedha ilizokopesha watu na taasisi mbalimbali.

Akizungumzia taarifa zinazoenezwa kwamba benki zimekosa fedha za kujiendesha, Mafuru alisema taarifa walizozipata ni kwamba Septemba mwaka huu, benki hizo zaidi ya 50 nchini zimekopesha zaidi ya shilingi trilioni 16.3 kwa watu mbalimbali.

Huku akisema kuwa kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 1.43 zimekopeshwa bila ya kurudishwa katika benki husika na kwamba benki hizo zinashindwa kueleza ukweli uliopo badala yake wanalalamika kwamba hatua ya serikali kuamua fedha zake zitunzwe BOT badala ya katika benki za kibiashara, ndio sababu ya hali yao benki mbaya.

Kwa mujibu wa Mafuru, serikali imeamua kuchukua uamuzi huo wa kuzitoa fedha zake kutoka katika benki mbalimbali za kibiashara nchini kwa ajili ya kuwezesha serikali kujua mapato wanayopata kutoka katika taasisi zake.

Msajili wa Hazina amesema zaidi ya Shilingi bilioni 515 zimeingizwa BOT baada ya uamuzi huo wa Serikali ya Awamu ya Tano ambao ulitangazwa na Rais John Magufuli baada ya kushika madaraka mwaka mmoja sasa. Mafuru alikiri kuwa ni kweli kwamba mzunguko wa fedha umekuwa mdogo na kueleza kuwa chanzo chake si kwamba benki zimekosa fedha kwa ajili ya kujiendesha.

Aidha Mafuru alisema kuwa awali watu wengi walitegemea safari na posho ambazo baada ya chenji kubaki, walikuwa wakitumia bila ya malengo, lakini sio kwamba mzunguko huo wa fedha unawaathiri watu wote.

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents