Naibu Waziri Ummy Nderiananga awaomba wadau kusaidia watoto wenye mahitaji maalum (+Video)

Serikali imesisitiza kwamba itaendelea kufanya jitahada mbali mbali katika kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika nyanja zote za uchumi na kutoa wito kwa wadau kutoa mchango wao katika kuwawezesha watu wenye ulemavu hususan watoto wadogo ili waweze kupata elimu na malezi bora yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao na hatimaye kutoa mchango wao katika maendeleo ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Watu Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga, alipokuwa akikabidhi vifaa mbali mbali vya msaada katika shule za watu wenye ulemavu ambavyo vimetolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, amesema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taasisi yake wa kusaidia jamii kwenye sekta za elimu, afya, majanga na uboreshaji wa mazingira ya kazi.

Aidha, wanafunzi na viongozi wa baadhi ya shule zilizopatiwa msaada wa vifaa hivyo, wameishukuru Taasisi ya OSHA kwa msaada uliotolewa na kuwaomba wadau wengine kuendelea kusaidia kutatua changamoto mbali mbali zinazozikumba shule za watoto wenye ulemavu.

Msaada huo wenye thamani ya takribani milioni 15, ambao ulihusisha ukaguzi wa usalama na afya hususan katika mabweni ya wanafunzi, umetolewa katika shule tatu za msingi za watoto wenye ulemavu za Uhuru Mchanganyiko ya Dar es Salaam, Mazinyungu ya Kilosa-Morogoro na Buigiri ya Chamwino jijini Dodoma. Miongoni mwa vifaa vilivyotolewa ni pamoja na; kompyuta, vifaa vya kuzimia moto, taulo za kike, vifaa kinga, vifaa vya usafi, karatasi na vibao maalum ya kuandikia watu wenye ulemavu.

Related Articles

Back to top button