HabariSiasa

Prof. George Luchiri mgombea Urais Kenya atakayehalalisha Bangi

Mgombea wa urais nchini Kenya kwa tiketi ya chama cha roots Prof. George Luchiri Wajackoyah anaendelea kuzua mjadala mkubwa kutokana na ahadi zake ambazo kwa wakenya wengi, zinaelezea uhalisi wa mambo lakini kwa baadhi yao, haziwezi kukubalika na katiba ya nchi hiyo wala maadhili ya Wakenya.
Manifesto ya Wajackoya ni ya kurasa mbili mbekee, lakini imezua mjadala mkubwa na kila mtu anamzungumzia.

Wajackoya anaangazia Zaidi namna ya kuinua uchumi wa Kenya kwa mda mfupi, labda miaka miwili baada ya kuingia madarakani.

Anaendelea kuwaambia wakenya kwamba inawezekana kulipa madeni yote wanayodaiwa kama taifa, na kuitajirisha nchi hiyo kwa mda mfupi sana kwa mutumia kilimo cha bangi, ufugaji wa nyoka, kuuza nyama ya mbwa na fisi.

Manifesto ya prof George Wajackoya inaangazia mambo 10.

Kenya kuwa miongoni mwa nchi tajiri duniani kutokana na kilimo cha bangi?

Kulingana na profesa Wajackoya ambaye amesomea sheria kuhusu uhamiaji, kilimo cha bangi ndio suluhisho kwa matatizo yote ya uchumi wa Kenya, na changamoto za kifedha kwa wakenya wote.

Anaamini kwamba Kenya itatajirika sana miaka miwili baada yake kuingia madarakani kutokana na kilimo chabangi.

Wajackoya amezua gumzo kote Kenya kutokana na msimamo wake kwamba bangi ina uwezo wa kulipa madeni yote ya Kenya katika mda mfupi, na gharama ya maisha kushuka kwa kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

Wakati wa kuzindua manifesto yake, Wajackoya alisema, “Tukilima bangi katika sehemu za Nyeri pekee, kila mkenya atapokea kiasi cha shilingi za Kenya 200,000 kila mwaka. Tukilima bangi Nyeri pekee, tutajenga barabara pana na za kisasa mbili katika kila kaunti (Kenya ina kaunti 47), hatutaomba pesa wala kukopa madeni kutoka kwa nchi zingine.”

Ameahidi pia kuwaachilia huru wafungwa wote waliopatikana na hatia ya kulima, kusafirisha au kuuza bangi nchini Kenya. Isitoshe, serikali yake itawalipa fidia ya shilingi milioni moja baada ya kuwaachilia huru.

“Ekari moja ya bangi italeta shilingi za Kenya milioni 16 kila mwaka. Chama cha Roots kitapata pesa za kutosha kutokana na kilimo cha bangi na kulipa deni lote la Kenya ndani ya mwaka mmoja. Bangi pekee itatosheleza bajeti nzima ya Kenya ya shilingi Trilioni 3.3.”

Katika kampeni, Wajackoya anaendelea kusisitiza kwamba “katika sehemu za mlima Kenya kahawa na majani chai vilisaidia sana sehemu hizo kuinuka kiuchumi kuanzia mwaka 1923, na kabla ya hapo, ilikuwa kinyume cha sheria kwa mtu yeyote Kenya kijihusisha na kilimo cha kahawa au majani chai. Kwa sasa bangi ndio mmea wenye faida kubwa duniani na wakenya wanastahili kujua kwamba matumizi ya bangi inaruhusiwa katika nchi zilizoendelea.”

Viongozi wa kidini hata hivyo wamekosoa ujumbe wa Wajackoya kuhusu bangi, wakisema kwamba anayosema “yanavunja kabisa sheria, maadili na utamaduni wa wakenya.”

Ufugaji wa nyoka wenye sumu kwa faida ya uchumi wa Kenya

Prof. Wajackoya vile vile anaendelea kuwaambia wakenya kwamba ufugaji wa nyoka wenye sumu unafaida kubwa sana ya kifedha. Kulingana na manifesto yake, sumu kutoka kwa nyoka itasafirishwa hadi nchini China na kutengeneza dawa za kutibu magonjwa ambayo hajaeleza.

“kila nyoka mwenye sumu ataleta dola 6,000 au shilingi za Kenya 600,000. Kila mkenya atapata dola 5,300 kwa kila nyoka anayeuza. Tutatumia ufugaji wa Nyoka kugharamia bajeti ya sekta ya elimu nzima,” amesema Wajackoya.

Kulingana na utafiti uliofanywa na madaktari Sanjoy Kumar pal, Aparina Gomes, SC Dasgupta, Antony Gomes na Dr. Liji Thomas na kuchapishwa katika maktaba ya utafiti kuhusu dawa – National library of medicine, sumu ya nyoka inatumika kutengeneza dawa inayotumika katika matibabu ya magonjwa sugu kama shinikizo la damu, ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa figo, kisukari, matatizo ya misuli, aina tofauti za saratani miongoni mwa mengine. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/12974396/ na https://www.news-medical.net/health/The-Medical-Uses-of-Venom.aspx

Uuzaji wa nyama ya mbwa na sehemu za uzazi za fisi

Kando na kilimo cha bangi na kufuga nyoka, Prof Wajackoya anadai kwamba bei ya nyama ya mbwa na sehemu za uzazi wa fisi ni ghali sana nchini China, na kwamba utawala wake utahakikisha kwamba wakenya wanafuga mbwa kwa wingi ili kujinufaisha na soko la nyama hiyo.

Kulingana naye, nyama hiyo ya mbwa na sehemu za uume wa fisi, vitachangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi wa Kenya.

“Hii ndio fursa pekee kwa wakenya kubadilisha hii nchi kiuchumi. Mimi na mgombea mwenza wangu ndio wenye sera za ukweli za kubadilisha hii nchi.” Amesema Wajackoya.

Mafisadi kuuawa

Katika utawala wa Wajackoya, watu wote watakaopatikana na makosa ya ufisadi watauawa. Adhabu hiyo itafanya wakenya kuogopa kujihusisha na ufisadi. Amesema kwamba watu wengi ambao wametuhumiwa kwa ufisadi nchini Kenya hawajachukuliwa hatua yoyote na wanaendelea kujihusisha na ufisadi, wengine wakiteuliwa serikalini.

“Adhabu kali kwa wanojihusisha na ufisadi litakuwa funzo kwa wengine. Hatua hii inatumika vyema sana nchini Singapore, China, Indonesia, Vietnam, Thailand, Iran na Morocco ambapo wanaopatikana na makosa ya ufisadi au kupokea hongo wanahukumiwa kifo.” Amesema Wajackoya.

Ameahidi kuweka sheria zinazowazuia maafisa wa serikali na wabunge kutofanya biashara na serikali, wala kumiliki vyombo vya Habari ili kuhakikisha kwamba kuna uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wa Habari wanalipwa vyema ili wawe huru kufichua mafisadi na maovu mengine.

“Jamii yetu imetawaliwa na fikra za kuwaabudu watu wenye pesa huku jamii ikiwa maskini. Hii inafanya watu walio madarakani kujinyakulia pesa nyingi ili waendelee kuabudiwa na kuheshimiwa zaidi ya wengine. Tabia hii inafanya wanaiba pesa za serikali ili kuendelea kuwa na sifa kwamba ni matajiri. Nitaweka sheria ya kuua mafisadi wote.”

Kufunga reli ya mwendo wa wastan SGR iliyojengwa na China

Licha ya ujenzi wa reli ya mwendo wa wastan ya Kenya SGR kuwa mradi ambao umeigharimu kiasi kikubwa cha pesa kwa kitita cha dola bilioni 3.6, Wajackoya amesema kwamba atafunga kabisa mradi huo atakapoingia madarakani. Kulingana na Wajackoya, reli hiyo hiyo ni ishara ya ukoloni na unawagharimu wakenya kiasi kikubwa cha pesa, akisistiza kwamba hauna faida yoyote.

“sanamu zote za wachina kwenye reli hiyo zitaondolewa na tujenge reli yetu, kwa mfumo wetu, kwa gharama yetu, bila kukopa. Reli ya wachina inatufanya tunaonekana kama tumetawaliwa. Ni ishara kamili ya kutawaliwa. Tunaonekana kama wakoloni wa China” amesema Wajackoya.

Ahadi za Prof Wajackoya kwa wakenya

Ukulima wa bangi kwa ajili ya kuuza nje ya nchi na kujenga uchumi wa Kenya, kulipa madeni na kuwatajirisha wakenya wote.
Kufuta mikataba yote kati ya Kenya na China
Kuuza nyama ya mbwa na fisi nje ya Kenya
Kuuwa watu wanaopatikana na makosa ya ufisadi
Kufunga reli ya kisasa iliyojengwa na China kwa gharama ya dola bilioni 3.6
Wafanyakazi wa serikali kufanya kazi siku 4 pekee kwa wiki. Siku 3 ni za mapumziko
Kutawala bila kutumia katiba
Kuhamisha makao makuu ya Kenya kutoka Nairobi hadi Isiolo
Kuunda serikali ya majimbo
Kufukuza raia wote wa kigeni wanaoishi Kenya na hawana kazi maalum.
Siku 3 za mapumziko kwa wafanyakazi wote Kenya

Prof George Wajackoya anataka wakenya kufanya kazi siku nne pekee kwa wiki, siku tatu za mapumziko.

Maelezo yake ni kwamba Ijumaa ni siku ya maombi kwa waumini wa dini ya kiislamu, na madhehebu tofuati ya wakristo hufanya maombi yao jumamosi na jumapili. Hivyo, anataka siku hizo tatu za maombi kuheshimiwa na kuwa likizo kwa kila mkenya.

Kuongoza Kenya bila kutumia katiba

Manifesto ya Wajackoya inasema kwamba ataongoza Kenya bila ya kutumia katiba “kwa sababu kuna baadhi ya sehemu za katiba hiyo anazodai hazina maana na zinairudisha Kenya nyuma kimaendeleo.”

Wajackoyah amesema kwamba kuna nchi ambazo zimeendelea bila ya kutumia katiba zilizoandikwa.

“Tuna nchi ambazo hazina katiba. Nchi kama Uingereza, Canada, Newzealand na Israel hazina katiba lakini uongozi wao ni mzuri sana. Wanatumia mahakama na bunge kufanya maamuzi yao.” Amesema Wajackoya, akiongezea “tutatunga sheria zinazokubaliwa na raia sio wanavyofikiria wanasiasa. Serikali ya Uingereza haiwezi kutunga sheria bila kuwashirikisha raia. Hapa Kenya, viongozi wanaamua tu na kuandika kurasa 260 za katiba na kutunga sheria za kuwaadhibu wakenya.”

Isiolo kuwa makao makuu ya Kenya, Nairobi kuwa mji wa viwanda

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa manifesto yake jijini Nairobi, prof Wajackoya alisema kwamba “mji wa Isiolo na miji iliyo karibu na mji huo ina ardhi kubwa ambayo serikali haijaweka katika matumizi yanayofaa.”

Isiolo ni mji wa kaunti ya Isiolo, katikati mwa Kenya. Mji huo unapatikana kilomita 285 kaskazini mwa mji mkuu wa Nairobi.

Wajackoya anataka Isiolo kuwa makao makuu ya Kenya kwa sababu upo karibu na jamii ya wasomali akisema kwamba “jamii hiyo imekandamizwa kwa miaka mingi sana Kenya.”

“Isiolo yakiwa makao makuu ya Kenya, waekezaji watawekeza sehemu hiyo na kuhakikisha kwamba inakuwa kwa haraka.” Amesema Wajackoya, akiongezea kwamba “Kila mtu anataka kuishi Nairobi. Mji umejaa, mazingira yamechafuka sana, mabomba ya maji chafu imejaa na yamezidiwa na kiwango cha uchafu. Mji umejaa kelele na hewa imechafuka. Watu wananyakua ardhi ya serikali na kujenga nyumba za kibinafsi.” Alisema Wajackoya.

Serikali ya majimbo

Manifesto ya prof Wajackoya inaahidi wakenya serikali ya Majimbo. Utawala wake utakuwa na majimbo 8 na kila jimbo litakuwa na utawala wake.

Kufukuza raia wote wa kigeni wasiokuwa na kazi

Akiwa profesa aliyesomea uhamiaji, na wakili anayetetea wahamiaji, Wajackoya amesema kwamba atawafukuza raia wote wa kigeni wasiokuwa na kazi maalum. Msako wa kwanza utawalenga raia wa China.

“Tutaanza kwa kuwafukuza wachina. Wachina wataenda kwao. zile zabuni ambazo wamepewa na serikali ya sasa nitazifutilia mbali kabisa. Kenya itajengwa upya.” Amesema Prof George Luchiri Wajackoya, mwenye umri wa miaka 63, shahada 16, mzaliwa wa Mumias, Magharibi mwa Kenya na mwenye ukoo wa jamii ya wasamia ambao wengi wao wanapatikana Kenya na Uganda.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents