Habari

Serikali yahitimisha zoezi la uhakiki wa NGO’s nchini

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto imehitimisha zoezi la uhakiki kwa Mashirika Masiyo ya Kiserikali nchini ulioanza Mwezi Agosti mwaka 2017.


Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi Sihaba Nkinga(kushoto) akizungumza na wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na waandishi wa habari Mjini Morogoro wakati akihitimisha zoezi la uhakiki wa NGOs nchini ulioanza Mwezi Agosti Mwaka 2017 kulia ni Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bw. Marcel Katemba
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW)

Akizungumza wakati wa kutoa taarifa kwa umma kuhusu kukamilisha zoezi hilo Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi Sihaba Nkinga amesema kuwa jukumu la Wizara ni kusajili na kuratibu shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mujibu wa Sera ya kitaifa ya Mashirikka Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini kwa kuimarisha mifumo ya uratibu kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini.

Bibi Sihaba Nkinga ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuzingatia Sheria, taratibu na kanuni zilizopo katika kuendesha kazi zao katika kuhudumia jamii.

“Tumekamilisha zoezi hili kwa kipindi tulichokiweka na ninawaomba wadau wetu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo katika utendaji wa shughuli zao la kila siku” alisema Bi Sihaba.

bibi Sihaba mefafanua kuwa Mashirika ambayo hayakuweza kuhakikiwa kwa sababu za msingi katika kipindi chote cha uhakiki, yanatakiwa kufika Ofisi ya Msajili wa NGOs ili kukamilisha zoezi hilo na mara baada ya tarehe hiyo muda wa uhakiki utasitishwa na mashirika hayo hayataruhusiwa kufanya kazi yoyote nchini kwa kushindwa kuzingatia taratibu.

Kwa upande wake Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini Bw. Marcel Katemba amewashukuru wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kwa kujitokeza kuhakiki Mashirika yao na kuwaomba kuendeleza ushirikiano uliopo kati yao na Serikali.

“Niwashukuru wadau wetu kwa kujitoa kwao na kuona umuhimu wa kushiriki na kuwa waangali wa zoezi hili la uhakiki wa Mashirika yao” alisema Bw. Katemba.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini Bw. Ismail Suleiman ameishukuru Serikali kwa kuendesha zoezi la uhakiki wa mashirikka hayo nchini kwa lengo la kusaidia kukuza ufanisi wa kazi zao.

“Tunaishukuru Serikali kwa zoezi hili ambalo litatusaidia kuendesha shughuli zetu kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo”alisema Bw. Suleiman.

Zoezi hili limefanikisha kuhakiki wa jumla ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 3,186 kati ya Mashirika 8,500 yaliyotarajiwa kuhakikiwa. Aidha, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 2,655 yamesajiliwa chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa mwaka 2005 na Mashirika 518 yamesajiliwa chini ya Sheria nyingine.

Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents