Habari

Serikali yavunja ukimya dili ya helikopta za Jeshi

WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa limesema haijawahi kuingia mkataba wowote na Kampuni ya Khaisa Enteprises kununua helikopta kutoka Ufaransa.

Na Beatrice Moses


WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa limesema haijawahi kuingia mkataba wowote na Kampuni ya Khaisa Enteprises kununua helikopta kutoka Ufaransa.


Akizungumza jana na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Abel Mwaisumo, alisema hakuna uhalali wa taarifa za madai zilizotolewa na Khaisa Enteprises Ltd hivyo wizara hiyo haiwajibiki kulipa fidia yoyote.


” JWTZ ni chombo cha wananchi na majukumu yake yapo kama yalivyoagizwa kikatiba, suala la kutumia ubinafsi na biashara zinazokinzana na sheria na taratibu zilizowekwa ili kukipaka matope ni kinyume na malengo ya ulinzi wa Taifa,” alisema Bw. Mwaisumo.


Alikiri kwamba ni kweli JWTZ ilikuwa na mahitaji ya helikopta kwa shughuli zake za kiulinzi na huduma kwa Taifa hivyo liliamua kuwasiliana na Kampuni ya Eurocopter ambayo ilipeleka wataalamu kwa utafiti zaidi nchini Ufaransa.


Bw. Mwaisumo, alisema kuwa hata hivyo gharama za ununuzi wa helikopta hizo ilikuwa kubwa na Wizara haikuweza kumudu hivyo kusitisha mradi huo ili kutafuta wafadhili wanaoweza kusaidia kuugharamia.


“Ukwasi uliendelea ambapo Eurocopter walipewa taarifa kwa barua kuhusu hali hiyo, nao wakapendekeza kupunguza idadi ya helikopta tulizohitaji kulingana na uwezo wetu wa kifedha, hata hivyo tuliwajibu kusitisha hadi tutakapopata ufumbuzi wa kifedha,” alisema Bw. Mwaisumo.


Alisema katika kipindi hicho hicho, ndipo Khaisa Enteprises ikaanza kufuatilia mradi huo mara kwa mara jeshini kama mwakilishi wa Eurocopter hapa nchini.


Katibu Mkuu huyo alidai kuwa ufuatiliaji huo wa Khaisa Enteprises, ulionekana kuwa kero na ulikiuka maadili ya utendaji kazi ambapo uongozi wa wizara, uliamua kutoa uamuzi na kuifahamisha Eurocopter kuwa mradi huo umefutwa.


Alisema baada ya uamuzi huo, Khaisa Enteprises ilianza kutapatapa na kuwasiliana na wizara kuomba isaidiwe kupata fedha zake kufidia gharama ilizotumia kutangaza biashara yake ya kuliingizia jeshi helikopta.


” Fedha anazodai kuwa ni fidia ni zaidi ya dola milioni moja, nilizungumza naye ili kujua uhalali wa fidia hiyo lakini hakuna, hii ni biashara chafu ambayo anataka kuifanya, tena tunaweza kumshitaki lakini tunaona kwamba tutakuwa tumemmaliza,” alisema Bw. Mwaisumo.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents