Burudani

Sparrow aachia ngoma mpya ‘Mawazo Nitulize’ aliyomshirikisha Barnaba K

Mapenzi ni kitu kinachotawala zaidi maisha ya binadamu duniani kote na wasanii kwa miaka mingi wamekuwa mstari wa mbele kutumia vipaji vyao kuwawakilisha watu wengine katika kufikisha ujumbe mzuri wa kimapenzi kwa wanaowapenda.

SPARROW 2

George Mgaya maarufu kwa jina la Sparrow, ameungana na muimbaji na mtunzi bora kabisa wa nyimbo katika kizazi hiki, Barnaba kutengeneza wimbo ‘Nitulize’ ambao licha ya kumtaka mrembo atulie na kuthibitishiwa penzi la dhati na nafasi yake ya kipekee kwenye mioyo yao, wimbo huu umebarikiwa na mdundo mkali unaochezeka.

Mpishi wa wimbo huu, Amiga Tyga wa Teyrano Music, hajakuacha uusikilize wimbo huu ukiwa umekaa tu na kukufanya ucheze hata bila hiari yako.

Sparrow ambaye kikazi anaishi mjini Dodoma anasema alikuja Dar es Salaam kurekodi wimbo na producer wa De Fetality, Mesen Selekta lakini ratiba zao zilipishana na hivyo kupitia rafiki yake, Malcom, alijikuta akishawishika kutaka kurekodi wimbo na Amiga Tyga baada ya kusikiliza wimbo aliomtengenezea rapper Bonge la Nyau.

“Amiga Tyga ni producer ambaye mimi nilikuwa namtafuta kitambo. Nilivyogundua kuwa ndiye producer aliyetengeneza hiyo ngoma, nikahisi kwamba anafaa na mimi kuweza kunitengenezea ngoma, nikasema basi ngoja nimtafute,” anasema Sparrow.

Sparrow anadai baada ya kutengeneza mdundo wa wimbo huo yeye na producer wake walishauriana kumshirikisha msanii mwingine ili kuweka ladha nyingine tamu na jina la Barnaba likapita miongoni mwa majina yaliyopendekezwa.

Sparrow anasema matarajio yake ni kuendelea kutengeneza muziki mzuri na kuwaacha mashabiki wao wenyewe waamue wanamweka kwenye nafasi katika muziki wa Tanzania.

“Natamani niwepo pale kama wengine waliopo hiyo sehemu na nafasi ambazo wamepewa na mashabiki wao. Na mimi pia nahitaji mashabiki wangu waniweke sehemu ambayo wamewekwa wasanii wengine,” anasisitiza rapper/muimbaji huyo ambaye anadai Jux na Belle 9 ndio wasanii anaowaangalia zaidi na anaopenda kufanya nao kazi siku za usoni.

Kwa wimbo huu Nitulize, hakuna shaka Sparrow anajiandalia nafasi yake mwenyewe ya kufurahia matunda ya kipaji chake cha muziki siku zijazo. Pata nafasi ya kuburudisha masikio yako kwa kusikiliza wimbo huu mtamu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents