HabariUncategorized

TCRA yatoa adhabu kali kwa vituo vitano vya Runinga, Habari za uchochezi zaelezwa

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imevipiga faini vituo vitano vya runinga nchini Tanzania kwa makosa ya kukiuka Kanuni za Huduma za Utangazaji, Maudhui za mwaka 2005.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TCRA, Joseph Mapunda

Vituo hivyo vilivyopigwa faini ni ITV, Azam TV, Star TV, Channel Ten na EATV kufuatia vipindi vyao vya taarifa ya habari vilivyoruka tarehe 30 Novemba 2017 katika nyakati tofauti tofauti.

Adhabu hizo zimekuja baada ya vituo hivyo vya Habari kurusha tathmini iliyotolewa na Kituo cha Haki za Binadamu juu ya uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika katika kata 43 mwaka jana 2017.

Soma zaidi tathmini hiyo iliyotolewa tarehe 30 Novemba, 2017 na Kituo cha Haki za Binadamu {Kituo cha Haki za Binadamu chaanika madudu yaliyojitokeza uchaguzi mdogo wa madiwani}

Akifafanua adhabu hizo leo Januari 2, 2018. Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TCRA, Joseph Mapunda amesema Vyombo vyote vya habari vilipewa nafasi ya kutoa utetezi wao kuhusu taarifa hizo walizotoa kabla ya Mamlaka hiyo kutoa adhabu leo.

Makosa yote yaliyovikumba vituo hivyo vya Runinga ni matatu ambayo ni Uchochezi, Kukiuka maadili ya uandishi wa habari na Habari zao kukosa mizania.

Habari zote zilizotolewa na vituo hivyo vya Runinga kuhusu tathmini ya Uchaguzi mdogo wa madiwani iliyotolewa na Kituo cha Haki za Binadamu zilieleza kuwa uchaguzi huo ulikuwa na vitendo na matumizi mabaya ya vyombo vya dola, matukio ya watu kutekwa na watu wasiojulikana, watu kupigwa, kukamatwa na kujeruhiwa kwa lengo la kuharibu na kuvuruga uchaguzi na kuwatia hofu wapiga kura.

Adabu za vituo vyote vitano ni kama ifuatavyo:

1-ITV

Kituo cha runinga cha ITV, kimetozwa faini ya jumla ya Tsh milioni 15, kwa makosa matatu ikiwemo, kukiuka maadili ya uandishi na kutangaza habari za uchochezi na faini hiyo inapaswa kulipwa ndani ya siku 30.

2-Azam Two

TCRA imekitoza faini ya TZS milioni 7.5 kituo cha runinga cha Azam Two, kwa makosa ya kutangaza habari za uchochezi, kutangaza habari ambazo hazikuzingatia maadili ya uandishi na kutozingatia mizania.

3-EATV

Kituo cha runinga cha EATV, kimetozwa faini ya jumla ya Tsh milioni 15, kwa makosa matatu ikiwemo, kukiuka maadili ya uandishi na kutangaza habari za uchochezi kwenye kipindi chake cha Hot Mix cha tarehe 30 Novemba 2017 .

4-Channel Ten

TCRA imekitoza faini ya Tsh milioni 15 kituo cha Runinga cha Channel Ten, kwa makosa ya kutangaza habari ambayo haikuzingatia maadili ya uandishi, kutangaza habari za uchochezi, na kutozingatia mizania.

5-Star TV

Kituo cha runinga cha Star TV cha jijini Mwanza, kimetozwa faini ya jumla ya Tsh milioni 7.5 kwa makosa matatu ikiwemo, kukiuka maadili ya uandishi na kutangaza habari za uchochezi.

TCRA imesema adhabu zote za faini zinapaswa kulipwa ndani ya siku 30 na vituo vyote vilivyotoa taarifa hizo za kichochezi vitakuwa chini ya uangalizi maalumu wa TCRA kwa miezi 6.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents