Habari

Uchaguzi kurudiwa nchini Kenya (+Picha)

Mahakama ya Juu nchini Kenya imefutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa Urais uliofanyika Agosti 8 mwaka huu, ambapo Uhuru Kenyatta alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Raila Odinga akiongea na waandishi wa habari mapema leo baada ya tamko la Mahakama

Maamuzi hayo ya mahakama yamekuja baada ya vyama vinavyounda umoja wa Upinzani (NASA), kupeleka malalamiko yao Mahakamani wakishutumu kudukuliwa kwa matokeo ya uchaguzi huo huku wakidai kuwa haukuwa wa huru na wa haki.

SOMA ZAIDI – Odinga kutinga mahakamani kupinga matokeo ya urais nchini Kenya

Hukumu hiyo imetolewa leo na jopo la majaji 6 na ilirushwa moja kwa moja kwenye vyombo vya habari nchini Kenya, imesema uchaguzi huo utarudiwa baada ya siku 60.

“Uchaguzi wa urais uliofanyika 8 Agosti, 2017, haukuandaliwa kwa mujibu wa katiba na sheria, hivyo matokeo yake ni batili. Natangaza kwamba Bw Kenyatta hakuchaguliwa na kutangazwa kwa njia inayofaa, agizo linatolewa na kuagiza Tume ya Uchaguzi kuandaa na kuitisha uchaguzi mwingine kwa kufuata katiba na sheria katika kipindi cha siku 60.“amesema Jaji Mkuu David Maraga.

Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga amesema maamuzi hayo yaliyotolewa na Mahakama ni ya kihistoria na ni mfano wa kuigwa kwa nchi za bara la Afrika, huku akiondoa imani kwa tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo IBEC.

NASA hatuna imani tena na IEBC, na hakuna wa kuzuia safari yetu ya Kaanan, tunaishukuru mahakama kwa kutoa uamuzi huo,“amesema Raila Odinga.

Maamuzi hayo pia hayajawafurahisha viongozi wa upinzani pekee bali hadi kwa wafuasi wao kwenye miji mikubwa nchini humo kama Nairobi, Mombasa, Kisumu na miji mingine (Picha na BBC).

Wafuasi wa upinzani jijini Nairobi

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa tarehe 26 Agosti 2017, baada ya Muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya (NASA) kuishtaki Tume ya Uchaguzi kufanya udanganyifu juu ya uchaguzi huo uliompa ushindi Uhuru Kenyata.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents