Habari

Ufaransa kumaliza shughuli za kijeshi eneo la Sahel

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametangaza kwamba operesheni za kijeshi za taifa hilo katika mapambano dhidi ya wanamgambo walio na itikadi kali katika ukanda wa Sahel zinafikia mwisho.

Mali Frankreich beendet die Operation „Barkhane“

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Paris kabla ya mkutano wa kilele wa mataifa saba yaliyoendelea kiviwanda ya G7, Macron amesema operesheni Barkhane itamalizika rasmi na itabadilishwa na ujumbe mwingine unaolenga kupambana na wanamgambo wa itikadi kali na utategemea zaidi washirika wa kikanda.

Kulingana na Macron, Ufaransa sasa itajielekeza zaidi katika kusambaza vikosi vyake katika ushirikiano wa pamoja na nchi za Umoja wa Ulaya, kama sehemu ya kikosi kazi kinachoitwa Takuba kinacholenga kuzidisha juhudi katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali.

Aidha rais huyo amezungumzia juu ya “mabadiliko ya kina” ya operesheni za kijeshi nchini Mali na katika nchi jirani, bila ya kutoa muda kamili lakini maelezo ya kina yanatarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwezi huu ikiwemo idadi ya wanajeshi wa Ufaransa watakaosalia.

“Mabadiliko haya yatatokea kupitia mfumo tofauti, ambao utamaanisha mfumo mpya. Hiyo ni kusema kumalizika kwa operesheni Barkhane kama operesheni ya nje, kutaruhusu ujumbe wa msaada na ushirikiano na majeshi ya kikanda na kuanzisha operesheni ya kijeshi ya kimataifa, ikijumuisha washirika wetu wote, na tukizingatia tu vita dhidi ya ugaidi.”

Frankreich Mali - Emmanuel Macron und Bah N'Daw

Uamuzi huo unakuja siku chache baada ya kanali wa jeshi la Mali Assimi Goita, kuchukua madaraka kufuatia mapinduzi ya rais wa pili ndani ya kipindi cha miezi tisa na kuongezaka ukosoaji wa baadhi ya serikali kujadiliana na wanamgambo.

Mapema mwezi huu, Macron alielezea hatua ya Mali kama “mapinduzi ndani ya mapinduzi” na kusitisha kwa muda operesheni za pamoja baina ya Ufaransa na vikosi vya Mali mnamo Juni 3. Kwa hivi sasa Ufaransa ina jumla ya wanajeshi 5,000 katika ukanda wa Sahel.

Afisa mmoja mwandamizi wa Ufaransa amesema utekelezaji huo utachukua miezi kadhaa ambapo kwanza Paris itafanya mazungumzo na washirika wake wa Ulaya na Afrika. Maelfu ya wanajeshi watasalia katika ukanda huo wakishiriki katika operesheni tofauti zikiwemo za ujumbe mpya.

Vikosi vya Ufaransa vimekuwepo nchini Mali tangu mwaka 2013 vilipoingilia kati mapambano ya kuwaondoa waasi katika udhibiti wa mikoa ya kaskazini. Operesheni hiyo ilipanuliwa na kuzijumuisha nchi jirani za Chad, Niger, Burkina Faso na Mauritania katika jitihada za kuleta utulivu katika ukanda wa Sahel.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents