Vigogo wa CUF, NLD nusura watwangane

Mtafaruku mkubwa uliibuka juzi katika hoteli ya Bwawani, visiwani Zanzibar baada ya baadhi ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) na NLD kutaka kutwangana wakati wa kikao

Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar



 


Mtafaruku mkubwa uliibuka juzi katika hoteli ya Bwawani, visiwani Zanzibar baada ya baadhi ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) na NLD kutaka kutwangana wakati wa kikao.

Wanasiasa hao walifikia hatua ya kutaka kutwangana kwa viti baada ya kutofautina kuhusu suala la wazee wa Pemba kutaka kisiwa hicho kijitenge.

Kikao hicho kilikuwa ni kati ya vyama vya siasa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Kufuatia tafrani hiyo, mkutano huo ulilazimika kuvunjwa ili kuepuha vurugu.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Bw. Khatib Mwinyichande, alilazimika kuchukua hatua ya kuuvunja mkutano huo baada ya hali ya hewa kuchafuka.

Aidha, mmoja wa wajumbe kutoka CUF, alimtaka Naibu Katibu wa NLD, Bw. Rashid Ahmed Rashid, kufuta usemi wake kuwa, wazee waliotaka Pemba ijitenge, walitumwa na CUF.

Akichangia hoja katika mkutano huo, Bw. Rashid alisema wazee waliokamatwa kisiwani Pemba, walibeba ajenda iliyopikwa na CUF, baada ya hatua za kuundwa serikali ya mseto kukwama.

Kiongozi huyo aliishutumu CUF kwa maelezo kuwa, matatizo yanayoikabili Zanzibar, yanatokana na ubinafsi wa chama hicho kuweka mbele maslahi yake bila kushirikisha vyama vingine.

Kauli hiyo ilionekana kuwakera viongozi wa CUF na Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mwasiliano ya Umma wa chama hicho, Bw. Salum Bimani kulazimika kusimama na kumtaka Naibu Katibu Mkuu huyo wa NLD afute usemi wake.

Alisema yeye kama Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho, hatambui kuwepo kwa mpango huo na kauli hiyo ni nzito na inaweza kukiathiri chama cha CUF.

Bw. Bimani alisema ana wasiwasi Naibu Katibu huyo wa NLD ametumwa ili kujenga mazingira yatakayosababisha CUF kifutwe na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Baada ya hapo, viti vilianza kunyanyuliwa huku mjumbe wa CUF akimtupia maneno makali kiongozi huyo wa NLD.

Kutokana na hali hiyo, Kamishna wa Tume hiyo na Waziri wa zamani wa Serikali ya Zanzibar, Bw. Said Bakar Jecha, alimshauri Mwenyekiti wa Tume kuuvunja mkutano huo kutokana na jazba zilizojitokeza.

Baadhi ya wajumbe walisikika wakitaka kudhibitiwa kwa viongozi hao, hasa kwa vile mkutano huo ulikuwa ukifanyika ghorofa ya nne, jambo ambalo lingeweza kuleta madhara iwapo jazba hiyo ingezidi kuendelea.

Wiki iliyopita, watu saba walitiwa mbaroni huko Pemba kwa tuhuma za kupeleka madai yao katika ofisi za Umoja wa Mataifa kutaka Pemba ijitenge.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents