Habari

Vijana EAC watakiwa kushiriki katika masuala ya kisiasa

VIJANA waliopo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wametakiwa kuwa na uthubutu wa kushiriki katika masuala mbalimbali ya kisiasa na kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi ili wawe tunu ya kuleta demokrasia .

Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam leo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe wakati akifungua mdahalo wa siku mbili uliyoandaliwa na EAC na kuwakutanisha wanafunzi 42 wa vyuo vikuu kutoka katika nchi saba zilizopo katika jumuiya hiyo.

Profesa Mdoe amesema ni wakati wa vijana kuwa na uthubutu wa kushiriki katika masuala ya uchaguzi, siasa na kuwa tunu ya kuleta demokrasia katika nchi zao.

“Vijana wengi mara nyingi wamekuwa wakiongea katika mitandao ya kijamii lakini kushiriki katika uchaguzi au kuwania nafasi za uongozi imekuwa ni shida, niwaombe shirikini katika michakato yote ya uchaguzi, katika kutiana hamasa na kutoa elimu kuhusiana na masuala ya demokrasia hii itawafanya mpate viongozi bora watakaoleta maendeleo katika nchi zenu,” amesema Profesa Mdoe

Aidha amesema kumekuwa na matumizi makubwa ya kidigitali na teknolojia ambayo yanatoa nafasi nzuri ya kutengeneza masuala ya usalama na amani lakini kama yakitumika vibaya yanaweza kuleta shida.

“Kwa kutumia teknolojia ya akili bandia ni rahisi hata watu kujitangaza wameshinda huku kiuhalisia siyo klweli, vijana ziombeni serikali zenu haya masuala ya kidigitali yaingizwe kwenuye sheria na taratibu mbalimbali za uchaguzi ili ikitokea ijulikane wanamshughulikia mtu sheria gani,” amesema Profesa Mdoe

Hata hivyo amesema kuwa ili Jumuiya ya Afrika Mashariki iweze kutengamaa vizuri lazima kuwepo kwa usalama na amani katika nchi hizo na kwamba jambo hilo linaweza kutokea endapo kwenye nchi hizo kutakuwa na demokrasia.

Naye Ofisa Mwandamizi Idara ya Siasa EAC, David Onen amesema mdahalo huo umekuwa ukifanyika kila mwaka na kwa mwaka huu umefanyika nchini Tanzania ukiwa na mada inayohusiana na utendamano wa Afrika Mashariki, kujenga demokrasia, umoja, amani, na usalama.

“Mdahalo huu ambao ni wa nane kufanyika umekusanya wanafunzi 42 ambao wametoka katika nchi ya Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Tanzania, Sudani ya Kusini, DRC Kongo,” amesema

Kwa uapnde wake balozi wa vijana kutoka nchini Kenya, Stetchy Marion amesema mdahalo huo ni wa muhimu kwao kwani inawafanya waweze kujiamini na kujisimamia katika mambo yao mbalimbali.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents