Burudani

Vute N’kuvute ya vituo vya redio inawanufaisha watangazaji wenye majina na kuwaacha wachanga hoi

Hakikuwa kitu kilichotarajiwa kwa Maulid Kitenge kuondoka Radio One, alikokuwa amejizolea umaarufu mkubwa na kuitumikia kwa takriban miaka 10 (kama sijakosea) na kuhamia EFM, kipindi ambacho ilikuwa bado changa kabisa.

shapeimage_8

Kuhama kwa Maulid aliyeongozana na Omari Katanga kuliwatikisa Radio One, hasa kwenye kipindi chao cha michezo. EFM waliitikisa pia Clouds FM kwa kumchukua Ibrahim ‘Maestro’ Masoud, nguli wa uchambuzi wa michezo aliyekuwa Clouds Media Group kwa muongo mmoja.

Maestro aliungana na Kitenge na Katanga kuimarisha kipindi cha michezo, E-Sports chenye wasikilizaji wengi kwa sasa. Watatu hao walianzisha kipindi cha kwanza cha Michezo, Sports Headquarters cha masaa matatu katika muda uliozeeleka kuwa na vipindi vya mambo ya jamii na burudani. Kipindi hicho kwa sasa kinasikilizwa mno jijini Dar es Salaam.

EFM walijipinda tena na kumnyofoa Gadner G Habash kutoka kwenye kipindi cha Maskani cha Times FM na kushika kipindi cha jioni, Ubaoni.

Clouds FM walitupa ndoano yao yenye chambo kinono kwa watangazaji wawili wa East Africa Radio, George Bantu na Kennedy The Remedy walionaswa na kujiunga na vijana wa mjengoni, kama wanavyojiita. Wakati huo huo pia Azam TV ilichukua watangazaji wengi mahiri kutoka kwenye vituo vya ITV, Clouds TV na Star TV.

Surprise nyingine kubwa ikaja kuwa ya Dina Marious kuondoka Clouds FM na kwenda kuanzisha kipindi cha Uhondo pale EFM ambacho tayari kimevutia wasikilizaji wengi. Kama haitoshi, EFM ilipeleka makucha yake pia Times FM na kumnyakua mtangazaji wa The Jump Off, Jabir Saleh aliyeanzisha kipindi kipya, Ladha 3600.

Hivi karibuni, watangazaji wa muda mrefu wa Clouds FM, Paul James na Gerald Hando waliondoka na kukiacha kipindi cha Power Breakfast kikichechemea na hakika limekuwa pigo la ghafla ambalo hata hivyo haliwezi kudumu sana. Tetesi mtaani zinadai kuwa nguli hao wanahamishia majeshi yao EFM na kwamba wanaenda kukipa nguvu kipindi cha asubuhi ambacho kwa sasa hakina nguvu kama vipindi vingine vya kituo hicho.

April 1, Clouds FM waliwasurprise wasikilizaji wake kwa kuwaleta waasisi wa Power Breakfast, Masoud Kipanya na Fina Mango ambao bado hakuna uhakika kama watarejea tena kuziba pengo lilioachwa na PJ na Hando ama walienda kuonjesha tu siku hiyo.

April 4, Clouds FM walipiga stunt kubwa kuliko kwa kumrejesha Gadner G Habash kutoka EFM. Hilo limekuwa pigo kubwa kwa EFM ambao licha ya kumchukua Mpoki kuongeza urojo kwenye kipindi chao cha Ubaoni, kuondoka kwa Captain kumewajeruhi na ni lazima wanahaha kusaka mbadala wake.

Vuta N’kuvute hii itaendelea kuwa kubwa zaidi kwenye zama za sasa za biashara ya redio hususan za Dar kwakuwa mambo yamebadilika. Sasa hivi majina yana nafasi kubwa zaidi katika kuvutia biashara na watangazaji mastaa wamekuwa brands ambazo zinataka zilipwe fedha nyingi.

Kwa watangazaji ambao wamegeuka kuwa ‘brand’ ni ngumu kuwasainisha mikataba ya mishahara ya utani kama ya zamani. Wengi wanaelewa thamani yao na wanafahamu kuwa makampuni yanawafahamu na yanatambua nguvu zao. Kwahiyo Vuta N’kuvute hii itawahusu aidha watangazaji wenye majina, masupastaa, waliogeuka kuwa brands ama watangazaji wasio na majina sana lakini wana uwezo mkubwa kupitiliza na ambao lazima wahustle sana.

Kiufupi usajili huu wa watangazaji unawanufaisha zaidi mastaa na kuwaacha watangazaji wachanga hoi bin taaban wakiendelea kulipwa mishahara midogo. Na utashangaa utofauti mkubwa uliopo kati ya mtangazaji staa na mtangazaji mchanga au asiye na jina. Kwa mfano mtangazaji staa anaweza kulipwa shilingi milioni 3 hadi 5 (kwa wenye ushawishi) na bonus juu, huku mtangazaji asiye na jina akilipwa laki 4 au kubwa sana laki 7! Na hii haiji tu hivi hivi kwasababu soko linalazimisha utofauti wa ulipaji.

Kwamba makampuni mengi sasa hivi yapo tayari kudhamini kipindi kinachofanywa na mtangazaji maarufu na mwenye ushawishi kuliko kinachoongozwa na mtangazaji asiyejulikana. Kwahiyo vituo vya redio vipo tayari kumlipa mtangazaji staa fedha yoyote anayotaka kwasababu vinajua ataingiza mkwanja mrefu.

“Changamoto ni watangazaji hawa watalipwa mamilioni ya pesa wakati watangazaji wadogo wataendelea kulipwa laki mbili na nusu. Watangazaji wadogo have to fight so harder to pave the way,” anasema Sherry Aljaffer kwenye Instagram.

“How will they survive? How will they grow? Media industry is too sophisticated but complex. Haitaki beginners… My lecturer used to say “In digital age, the world is too capitalistic. Beginners are paid highly in prostitution and sex industry but not in other sectors”…Now I believe, it was true!,” ameongeza.

Ni kweli, watangazaji wachanga na wasio na majina wanatakiwa kufanya kazi maradufu ili kufaidi pia Vuta N’kuvute hii lasivyo wataendelea kulipwa mishahara midogo itakayowakatisha tamaa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents