Habari

Watu 15 wadaiwa kufariki baada ya mlipuko mkubwa kutokea Equatorial Guinea (+ Video)

Watu takriban 15 wamefariki dunia huku wengine zaidi ya 100 wakipata majeraha katika mfululizo wa milipuko iliyotokea nchini Equatorial Guinea, Wizara ya afya imesema.

Baadhi ya watu 500 walijeruhiwa kufuatia milipuko hiyo iliyotokea karibu na kambi za wanajeshi mji mkuu wa Bata Jumapili.

Milipuko hiyo imesababishwa na “uzembe” uliohusishwa na hifadhi ya baruti kali kambini, rais amesema.

Picha kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha moshi mkubwa na uharibufu uliotokea.

Televisheni inayomilikiwa na serikali imeonesha watu wakitafuta manusura katika vifusi huku wakiinua vipande vya majengo yaliyoporomoka.

Rais Teodoro Obiang Nguema amesema katika taarifa kwamba athari iliyotokana na mlipuko huo “imesababisha uharibifu mkubwa katika karibu nyumba zote na majengo huko Bata”, na kutoa wito wa usaidizi wa kimataifa na msaada.

Aliongeza kwamba huenda tukio hilo limetokea kufuatia hatua ya wakulima kuchoma mashamba yanayozunguka kambi za jeshi.

Katika mfululizo wa ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa Twitter, waziri wa afya aliomba wahudumu wa afya kujitolea na kwenda katika hospitali ya eneo la Bata. Pia imetoa wito watu kujitolea kutoa damu kwasababu ya idadi kubwa ya waliojeruhiwa.

Iliorodh! esha hospitali tatu ambako waliojeruhiwa sana wanapelekwa.

Baadhi ya hospitali za eneo zimepokea wagonjwa kupita kiasi, TVGE imeripoti.

Televisheni hiyo ilionesha picha za watu waliojeruhiwa wakiwa wamelala kwenye sakafu ya hospitali moja iliyojaa watu.

Video iliyowekwa katika mitandao ya kijamii baada ya kutokea kwa milipuko hiyo inaonesha watu waliochanganyikiwa wakitoroka eneo hilo huku moshi mkubwa ukiendelea kutanda kwenye anga.

“Tumesikia mlipuko na sasa tunaona moshi, lakini hatujui kinachoendelea,” mkaazi mmoja wa eneo amezungumza na shirika la habari la AFP.

Katika mtandao wa Twitter, balozi wa Ufaransa Olivier Brochenin ametuma risala zake za rambi rambi kwa waathirika, akizungumzia ajali hiyo kama “janga”.

Ramani ya mlipuko equitorial Guinea

Ubalozi wa Uhispania umesema kuwa raia wa nchi yake wasalie nyumbani na kutoa nambari kadhaa za simu za dharura.

Equatorial Guinea ilitawaliwa na Uhispani hadi ilipojipatia uhuru wake mnamo mwaka 1968.

Bofya hapa chini kutazama.

https://www.instagram.com/tv/CMJeT9rBDRu/

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents