HabariSiasa

Waziri Mkuu Majaliwa: Tunalichukulia kwa umakini suala la Loliondo

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema zoezi la uwekaji vigingi katika eneo la kilomita za mraba 1,500 la pori Tengefu la Poloreti, Loliondo mkoani Arusha ambalo limekamilika kwa asilimia mia moja halitoathiri maendeleo ya wakazi wanaoishi kwenye eneo la vijiji 14 vinavyopakana na eneo hilo.

Amesisitiza kuwa hakutakuwepo na kijiji chochote
kitakachofutwa na hakuna miundombinu itakayoondolewa kwa kuwa ndani ya eneo la kilomita za mraba 1,500 hakuna miundombinu yoyote.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akiahirisha mkutano wa saba wa bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema  serikali imesimamia kwa umakini zoezi la uwekaji vigingi kwenye eneo hilo ambalo ni muhimu kwa ikolojia ya hifadhi ya Serengeti na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, serikali imeendelea kushirikiana na wananchi wa Loliondo katika kuboresha malisho ya mifugo, uchimbaji wa visima vya maji, ujenzi wa majosho pamoja na miundombinu ya kunyweshea mifugo kwenye eneo la kilomita za mraba 2,500.

“Pia, ninaielekeza wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa sheria ya ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999 inatumika ipasavyo kutenga na kuweka mipaka ya vijiji.” ameagiza Waziri Mkuu

Amesema  serikali kwa kuzingatia matakwa ya wananchi hasa maeneo ya malisho kwenye vijiji 14 vilivyopo karibu na pori tengefu la Poloreti, itaweka utaratibu utakaopangwa kwa pamoja baada ya kukamilisha zoezi la utambuzi wa mifugo kwenye vijiji husika.

Kuhusu zoezi la wakazi wa Ngorongoro kuhama kwa hiari katika eneo hilo kwa ajili ya kupisha uhifadhi endelevu, Waziri Mkuu amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika kusimamia utekelezaji wa zoezi hilo na kwamba hadi kufikia tarehe 9 mwezi huu jumla ya kaya 293 zenye watu 1,497 zimejiandikisha.

Pia Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza wizara ya Maliasili na Utalii isianze zoezi upandishwaji hadhi wa maeneo ya mapori tengefu kuwa mapori ya akiba hadi wananchi watakapotoa maoni yao.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents